Header Ads Widget

MWANACCM AMWANDIKIA BARUA MWENYEKITI WA CCM TAIFA KUTAKA UTARATIBU WA KURUDISHA MAJINA MATATU


BARUA YA  KWANZA YA WAZI KWA MWENYEKITI WA CCM TAIFA SAMIA SULUHU HASSAN


YAH. MAONI YA KUBADILISHA UTARATIBU WA KURUDISHA MAJINA MATATU

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Husika na kichwa cha barua hapo juu

Kutokana na Idadi ya wananchi kuongezeka, Chama chetu pia kimeongeza Idadi ya wanachama wengi wenye sifa na uwezo wa kushika nafasi mbalimbali za Uongozi, 


Lakini pia idadi ya wasomi nayo imeongezeka hivyo sasa hivi tuna rasilimali watu kubwa,


Idadi hii kubwa inapelekea pia kuwa na wanachama wengi wanaowania nafasi za Uongozi, 


Hapo awali wanachama waliokuwa wakiwania nafasi za Uongozi walikuwa wachache na hata wengine walikuwa wakishawishiwa kuombwa kugombea hivyo ilikuwa ni rahisi kuchuja na kupata majina matatu ya wanachama watakaokwenda kupigiwa kura,


Lakini sasa hivi hali imebadilika

Imefikia hatua mamia na huenda hata maelfu ya wanachama wakajitokeza kuomba ridhaa ya kuwania nafasi za Uongozi hivyo si rahisi kwa majina matatu tu kutosha kumpata mtu sahihi anayestahili kuongoza na zipo sababu,


1) Jina la kwanza ni muhimu kupitishwa Kiongozi aliyepo madarakani ili atetee nafasi yake


2) Jina la pili ni muhimu kupitisha jina la mgombea kwa kuzingatia usawa wa Kijinsia (Gender)


Hivyo inabaki nafasi moja tu ya mgombea kwa hawa wanachama wote wanaogombea,


Kimsingi nafasi moja hii ni finyu mno kwa wanachama hususani wanachama wale wasio na Viongozi wanaoweza kuwasemea kwenye Vikao,


Si hivyo tu,

Kipindi cha Uchaguzi ni kipindi kizuri sana kwa Chama kuona vipaji vipya vya Uongozi,


Kupitia Chaguzi tunaona vipaji vya mikakati, vipaji vya maono, vipaji vya kusema kwa wanachama wanaogombea n.k


Hivyo ikiwa tutatumia utaratibu huu wa kurudisha majina matatu vipaji vyote hivi hatutaweza kuviona na huenda wengine wakakata tamaa na kuachana kabisa na Siasa na wengine wakahamia vyama vya Upinzani kutafuta fursa ya kugombea na kuwatumikia wananchi,


Utaratibu huu wa majina matatu utakifanya Chama kionekane ni cha watu wachache, familia chache watakaosemeana wenyewe kwenye vikao na wengine wajione sio sehemu ya CCM kwasababu ya kukatwa majina yao na kupitishwa wachache wanaojulikana na wanaotokea familia zinazojulikana hivyo itapelekea Chama kupunguza Idadi kubwa ya wafuasi na wanachama ambao watatafuta fursa katika vyama vingine,


Utaratibu huu wa majina matatu unaondoa haki ya mwanachama ya Kuchagua na kuchaguliwa, 


Kwasababu wajumbe wanaweza kuletewa majina matatu ya wanachama ambao si chaguo lao, 

Hivyo haki yao ya kuchagua itakuwa imepokwa,


Vilevile pia wanachama watakaokatwa majina yao watakuwa wameondolewa haki yao ya Kikatiba ya kuchaguliwa, 


Utaratibu huu wa majina matatu unakwenda kuminya Demokrasia ndani ya Chama kwasababu utazuia wanachama wengine kuonekana, kupata fursa ya kugombea na kupata fursa ya kumchagua Kiongozi wanayemtaka,


Utaratibu huu wa kurudisha majina matatu unapunguza nguvu ya maamuzi ya wanachama na kuvipa vikao nguvu ya kuwaamulia na kuwachagulia wanachama Viongozi wao,


Utaratibu huu wa majina matatu unaua Vijana na vizazi vijavyo vya kisiasa kwasababu kwa kiasi kikubwa hivi havijulikani na vikao vya maamuzi bali vinapambana kutafuta kuonesha vipawa vyao,


Kipindi cha Uchaguzi ndicho kinakuwa kipindi kizuri sana kwa kizazi hiki kipya kuonekana hivyo utaratibu wa majina matatu unakwenda kukizika rasmi kizazi hiki kisionekane,


Siasa ni mchezo wa fitna

Viongozi waliopo madarakani pia nao wanaweza wakafanya fitna ili wanachama wenye nguvu wasipitishwe kugombea nao,  


Hili tumelishuhudia maeneo mengi ambapo inafikia hatua wanachama wanaamua kumchagua mtu dhaifu ilimradi tu wamuondoe Kiongozi aliyepo madarakani, 


Siasa ni uwekezaji wa muda mrefu wa hali na mali hivyo ikiwa hawa wanachama waliowekeza kwa wananchi wao kisha wakaja kukatwa majina yao lazima itakwenda kuhatarisha mno Uhai wa chama na kupelekea mipasuko mikubwa kwenye Chama, 


Tuutumie Uchaguzi wa mwaka 2015 kama rejea lilipokatwa jina la Mh. Edward Lowassa ilipelekea kuwepo na mpasuko mkubwa ndani ya Chama,


Tumeona huko nyuma,

Wanachama wanapoletewa majina ambayo sio machaguo yao waliamua kushirikiana na vyama pinzani kukihujumu chama,


Tumeona kuna wanachama ambao walikuwa Viongozi wazuri lakini walipokatwa walikwenda Upinzani na hatimaye tukapoteza Chaguzi mbalimbali, 


Ili yasitokee haya ni vema chama kikatafakari upya kuhusu mfumo huu wa majina matatu,


Naomba ikikipendeza Chama kiongeze majina walau yawe kumi (10) kutokana na wingi wa wanachama wanaoomba kuwania nafasi za Uongozi,


Ama chama kikiona inafaa kipitishe wanachama wote kugombea kisha vikao viamue kuhusu majina matatu miongoni mwa wanachama watakaoongoza kwa kura,


Uchaguzi wa mwaka 2020 binafsi niliwania Ubunge kura hazikutosha nilikuwa mtu wa tatu kwa kura,


Lakini kama ungekuwa utaratibu wa chama kuleta majina matatu naamini kwa asilimia zaidi ya mia moja jina langu lisingepitishwa na wala lisingedhaniwa kama ni jina ambalo linaweza kuleta ushindani na kuwa watatu kwa kura,


Utaratibu huu wa majina matatu umetukatisha tamaa na kuturudisha nyuma wanachama wengi tulio na nia ya kuwania nafasi mbalimbali za Uongozi,


Kwa kuwa chama chetu ni sikivu na kinajali mno wanachama wake na kinafanya Siasa kulingana na wakati,


Ni matumaini yangu makubwa kuwa maoni haya yatazingatiwa na marekebisho yenye tija yatafanywa kwa ajili ya kuboresha na kukiimarisha chama chetu!


Wako katika ujenzi wa Chama cha Mapinduzi na Taifa la Tanzania 

IBRAHIM JEREMIAH

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI