MUKAMA Nyaonge, mkulima wa Pamba namba moja Mkoani Mara ambaye ni mkazi wa kijiji cha Bulendabufe, kata ya Igundu, Tarafa ya Nansimo, wilaya ya Bunda akiwa shambani kwake akijiandaa kunyunyizia dawa ya kuuwa wadudu.
Na COSTANTINE MATHIAS, Bunda.
MUKAMA Nyaonge, mkulima wa Pamba na mkazi wa kijiji cha Bulendabufe, kata ya Igundu, Tarafa ya Nansimo, wilaya ya Bunda Mkoani Mara, katika msimu wa kilimo 2023/2024 ameibuka mkulima namba moja na kinara wa uzalishaji wa Pamba.
Akiongea na Waandishi wa Habari za Pamba, Mkama amesema huko nyuma alikuwa anapanda zao la Pamba kawaida, lakini baada ya kupewa elimu ya kupanda kitaalamu amepata Mafanikio makubwa katika zao la Pamba pamoja na matumizi ya mbolea ya asili.
Anaeleza kuwa kupitia elimu hiyo, shamba lake linapata matunda mengi na msimu wa kilimo 2023/2024 alipata mavuno ya kilo 1,560 kwenye ekari moja ikilinganishwa na huko nyuma alipokuwa anapata kilo 700 mpaka 800.
Mzee Nyaonge anaishukuru serikali kupitia wataalamu wake huku akibainisha kuwa endapo hali ya hewa itakwenda vizuri atapata mavuno ya kutosha kuliko mwaka jana.
"Baada ya kutangazwa kuwa Mkulima Bora wa Mkoa wa Mara, nilifurahi sana kutokana na uzalishaji wangu wa Pamba kwenye eneo dogo...nilipokea kiasi cha shilingi Mil. 3 kama zawadi kutoka serikali baada ya kuwa Mkulima bora, ninashukuru sana kupata zawadi na nimejitahidi kuongeza mashamba kutoka ekari moja hadi kuwa tatu ambazo zimepanda kitaalamu," anasema.
Kutokana na zawadi hiyo, Mzee Nyaonge anasema amenunua mabati ya kuezekea nyumba na pia ameboresha Kilimo cha Pamba kwa kuweka vibarua ili kurahisisha shughuli za Pamba huku akitarajia kupata kilo zaidi ya 4,500 kwa ekari tatu.
Afisa Kilimo wa Kata ya Igundu, Simeo Nkwabi amesema Pamba ni zao la Biashara katika Mkoa huo na kwamba limewatoa wakulima kwenye Umaskini na kuweza kujikwamua kiuchumi na watoka kwenye Kilimo cha kujikimu na kufikia Kilimo cha kibishara.
Mratibu wa zao la Pamba wilaya ya Bunda, Mashaka Mashimba amesema Bodi ya Pamba imewezesha wakulima wawezeshaji kupata Baiskeli, Matrekta, Maboza, ndege nyuki ambazo zimerahisha shughuli ya Kudhibiti wadudu wanaoshambulia zao la pamba.
"Wilaya ya Bunda ina Wakulima 13,820 waliosajiliwa, tuna ekari 24,560 zilizolimwa Pamba katika wilaya yetu...tunaendelea kuhamasisha wakulima kupitia huyu mkulima Bora ili waongeze tija ya Pamba" amesema Mashimba.
Mwisho.
0 Comments