Na COSTANTINE MATHIAS, Maswa.
Kutokana na kuanza kushamiri Kwa matumizi ya mbolea hai Kwa wakulima wa Pamba nchini, mbolea hiyo imeonyesha matokeo chanya Kwa kurutubisha udongo na kulinda Afya ya mmea wa Pamba na kuongeza uzalishaji wa vitumba.
Hayo yamebainishwa jana na wakulima wa Pamba wilayani Maswa Mkoani Simiyu kwenye mahojiano na waandishi wa Habari, ambapo wamesema Mbolea hai imeongeza mavuno, lakini pia malighafi zake zinapatikana kwenye makazi ya wakulima.
Lupande Nilla, Mkulima kutoka Kijiji cha Senani amesema Mbolea hai haina gharama ikilinganishwa na mbolea za viwandani (Mbolea ya Minjingu) na kwamba vitumba vya Pamba vimeongezeka na pia mimea ya Pamba imekuwa na virutubisho vingi.
"Gharama ya mbolea hai ni nafuu, majani yana ukijani sababu kuna Nitrojeni nyingi sana ambayo inatokana na mbolea hai... uzalishaji wa vitumba ni Mkubwa na vingi, awali kwenye mmea mmoja tulikuwa tunapata vitumba 10 mpaka 15 lakini sasa tunapata vitumba 80 mpaka 100 na uzalishaji ni Mkubwa" amesema Lupande na kuongea.
"Mwaka jana ekari moja nilizalisha kilo 1800 na mwaka huu natarajia kupata kilo 2000 kwa ekari moja sababu vitumba vimeongezeka, lakini Maafisa Ugani kupitia Jenga Kesho Bora (BBT) wametufundisha mbinu nyingi za kupambana na wadudu na wanatembelea wakulima mara kwa mara".
Ameongeza kuwa mbolea hai inarutubisha udongo sababu ikimwagika kwenye udongo inaongeza virutubisho tofauti na mbolea ya viwandani yenye kemikali, mbolea hiyo inaweza kuchanganywa na sumu zingine ili kudhibiti wadudu wanaoshambulia zao la Pamba
Anastazia Joseph, mkulima wa Pamba Kijiji cha Senani amesema tangu waanze kutumia mbolea ya asili wameanza kupata mavuno kutokana na Pamba kuwa na vitumba vingi hali inayowafanya kuongeza mavuno na kupata tija.
Amesema huko nyuma mavuno yalikuwa haba, hata nyakati za ukame mbolea hiyo imesaidia mimea ya Pamba kutosinyaa na badala yake inaendelea kunawiri huku wakulima wengine wamekuwa wakijifunza kupitia mashamba yaliyotumia mbolea hai.
Afisa Ugani kupitia Mpango wa Jenga Kesho Bora (BBT) Haroun Jonas anayesimamia Kijiji cha Senani amesema walianza kuwahamasisha wakulima juu ya matumizi ya mbolea hai ili kuongeza Afya ya Udongo na baada ya kupata matokeo wakulima wengi wamepata mwamko.
"Mwaka jana kulikuwa na mvua kubwa na mashamba mengi yaliathiriwa, lakini wakulima waliotumia mbolea hai walipata matokeo mazuri ikiwemo Ongezeko la vibahasha na vitumba...mbolea hii inatumia malighafi ambazo zinapatikana kwa wakulima ambavyo ni Mkaa, Majibu, Sukari guru na Micronutrients ambazo zinatolewa na Bodi ya Pamba" amesema Haroun.
Amesema kabla ya Matumizi ya mbolea hai, uzalishaji ulikuwa mdogo kwani mkulima alikuwa anapata vitumba 15 mpaka 20 lakini baada ya matumizi ya mbolea hiyo imeongezeka kuanzia vitumba 80 mpaka 100 na rangi ya mimea au majani haikuwa na ukijani kutokana na kuathiriwa na Maji au ukame.
Amewataka wakulima wa Pamba kuchangamkia mbolea hiyo ili kuongeza uzalishaji sababu awali Wakulima walikuwa wanapata kilo 150, 200 mapaka 300 na wakulima waliozingatia mipulizo yote alikuwa anapata kilo 800 mpaka 1000 kwa ekari moja.
Mwisho.
Anastazia Joseph, mkulima wa Pamba Kijiji cha Senani wilayani Maswa akikagua shamba lake ambalo amelima kwa kutumia mbolea hai.
Lupande Nilla, Mkulima kutoka Kijiji cha Senani wilayani Maswa akikagua shamba lake ambalo limelimwa Kwa kutumia Mbolea hai.
0 Comments