Na Fadhili Abdallah, Kigoma.
WAKALA wa Nishati Vijiji (REA) inatarajia kugawa majiko banifu 200,000 kwa bei ya ruzuku ili kuunga mkono kwa vitendo mpango wa serikali wa matumizi ya nishati safi za kupikia ambazo haziathiri afya za watu wala kuharibu mazingira.
Mtaalam wa Nishati na Masuala ya jinsia kutoka REA, Joseph Sambali amesema hayo wakati wa hafla ya kugawa bure majiko 400 kwa Mama lishe na walengwa wa kusaidia kaya masikini (TASAF) ikiwa ni uhamasiashaji jamii wa matumizi ya nishati ambazo ni rafiki wa mazingira na afya za watu ikiwa ni kutekeleza mpango wa serikali wa kuhakikisha asilimia 90 ya watanzania wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.
Amesema kuwa kwa kawaida jiko moja linapaswa kuuzwa kwa shilingi 55,000 lakini baada ya serikali kuweka ruzuku majiko hayo yatauzwa kwa shilingi 10,000 kila moja na kwamba kipaumbel kitatolewa kwa makundi maalum hasa vijijini ambako matumizi ya kuni na mkaa ni makubwa.
Akikabidhi majiko hayo kwa walengwa Mbunge wa jimbo la Kigoma mjini, Kilumbe Ng’enda amesema kuwa serikali ya Raisi Samia imedhamiria kuiondoa Tanzania katika matumizi ya nishati chafu na ndiyo maana miradi mbalimbali inatekelezwa ikiwemo kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa kutumia majiko Banifu kwa Mama Lishe na Walengwa TASAF ili kuchochea matumizi hayo.
Baadhi ya walengwa walionufaika na majiko hayo akiwemo Zubeda Almas mlengwa kutoka kundi la wanufaika wa mpango wa kunusu kaya masikini ameishukuru serikali ya Raisi Samia kwa matendo ya huruma na kuona namna ya kuwasaidia watu wa kipato cha chini kuweza kuwa sawa na watu wengine.
Naye Mama Lishe, Leah Michael amelazimika kupiga magoti kuonyesha kwa vitendo shukrani yao kwa Rais Samia kuwezesha watu wa kipato cha chini kupata majiko banifu bila gharama ili kuunga mkono matumizi ya nishati safi ambapo wameahidi kuwa mabalozi wa kutangaza na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mwisho.

0 Comments