Header Ads Widget

DCEA YAMNASA KINARA WA MIRUNGI , YATEKEZA EKARI 285.5 SAME

 


Na Matukio Daima Media, Kilimanjaro 

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, imefanya msako maalum wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, inawashilia watu Saba akiwamo kinara wa biashara ya mirungi na kufanikiwa kuteketeza Ekari 285.5 za mashamba ya aina hiyo ya dawa za kulevya.

Msako huo ulioanza Machi 19 Hadi 25,mwaka huu ulifanikisha kumkamata kinara wa biashara hiyo Interindwa Zinywangwa Kirumbi maarufu kama mama Dangote aliyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu.

Akizungumza baada ya kukamilisha msako huo, Kamishna Jenerali wa DCEA,  Aretas Lyimo, amesema kwamba  mama Dangote ni, mzalishaji na msambazaji mkubwa wa dawa za kulevya aina ya mirungi nchini. 

Kwa zaidi ya miaka 30, anaendesha mitandao ya biashara haramu ya mirungi na kusimamia masoko ya dawa hizo za kulevya mahali tofauti nchini,  huku akijua kuwa ni kinyume cha sheria.

"Mwaka juzi Mamlaka ilifanya msako katika Wilaya hii, tulitoa elimu kwa wananchi ili waachane na kilimo cha mirungi na badala yake wajikite katika kilimo cha mazao mbadala pamoja na ufugaji.




“Pia tuliteketeza  ekari 535 za mashamba ya mirungi, chini ya ushirikiano na uongozi wa wilaya, tulitoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya dawa za kulevya, ikiwemo mirungi. Lengo lilikuwa kuwawezesha wakazi wa eneo hili kujikita katika kilimo cha mazao mbadala na ufugaji kama njia ya kujiongezea kipato” alisema Kamishna Lyimo.

Pia, Kamishna Lyimo alieleza kuwa, pamoja na jitihada hizo, uongozi wa wilaya ya Same na Wizara ya Kilimo na mifugo waliwapelekea wananchi wa maeneo hayo miradi ya ufugaji wa nguruwe na kugawa miche ya kahawa, iliki na mazao mengine.
Kutokana na juhudi hizo, wananchi wengi wameachana na kilimo na mirungi na kuanza kulima mazao mbadala, japo wapo wananchi wachache waliokaidi na kuendelea na kilimo na biashara ya mirungi.

 Kamishna Lyimo amesisitiza kwamba Mamlaka itaendelea kufanya operesheni kuhakikisha wananchi wote wanaojihusisha na biashara ya mirungi wanakamatwa na hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yao. 

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunatokomeza biashara na matumizi ya mirungi hapa nchini hasa ikizingatiwa kuwa, eneo hili la Same ni kitovu cha uzalishaji mirungi nchini hali inayohatarisha ustawi wa taifa letu ndio maana tunafanya operesheni hizi endelevu nchi nzima kuhakikisha tunadhibiti uzalishaji,usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya za mashambani na viwandani ili zisiendelee kuathiri wananchi” alisisitiza Kamishna Lyimo.



Kwa upande wake Agness Mshana mtendani wa kata ya Ekondi amekiri kutambua uwepo wa watu wanaojihusisha na kilimo cha mirungi na wao kama serikali wameendelea kutoa elimu juu ya madhara ya mirungi ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kupata mazao mbadala ili kuepukana na kilimo hicho.

“Tumejitahidi kuwaletea mradi wa nguruwe pamoja na miche ya miparachichi na kuwapa elimu ya madhara ya dawa za kulevya kwa maana mirungi inamadhara mengi yakiwemo kuchanganyikiwa, kupoteza nguvu za kiume, kushindwa kuhudumia familia vizuri, kupata kansa na kadhalika” alisema Agness

Naye Mkazi wa Kata ya Tae aliyejitambulisha kwa jina moja, Hawa alisema, hafahamu sababu ya watu kuendelea kujihusisha na kilimo cha mirungi kwani, kuna mazao mengi yanayostawi kama vile vitunguu, karoti na iliki pamoja na miradi ya nguruwe iliyoletwa na serikali. 

Aidha, ameiomba serikali kuimarisha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa mazao yanayozalishwa kupelekwa sokoni, hali itakayosaidia wananchi kuwa na uhakika wa masoko ya mazao yao na hivyo kuachana na biashara ya mirungi.  

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya inatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za wazalishaji, wasambazaji, na watumiaji wa dawa za kulevya. Ushirikiano huu utasaidia kutokomeza kabisa biashara hii haramu na kulinda ustawi wa jamii. Serikali itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika ili kuhakikisha Tanzania inakuwa taifa salama na lenye maendeleo endelevu.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI