By Malisa GJ,
Kwanza, ieleweke kuwa hili si jambo geni. Hii si mara ya kwanza kununua umeme nje ya nchi. Tunanunua umeme kutoka Zambia kwa ajili ya mkoa wa Rukwa, kutoka Uganda kwa ajili ya mkoa wa Kagera, na kutoka Kenya kwa ajili ya wilaya ya Mkinga, Tanga.
Pili, watanzania tunahoji kwanini tununue umeme nje wakati tuliambiwa bwawa la Nyerere likikamilika tutakuwa na umeme wa kutosha na tutaweza kuuza nje. Je, tulidanganywa?
Ili kujibu swali hilo ni muhimu kujua hali ya uzalishaji wa umeme nchini na vyanzo vyake. Vyanzo vya umeme wa maji (hydroelectric power plants) tulivyonavyo vina uwezo ufuatao:
- Kidatu inazalisha 204 MW
- Kihansi 180 MW
- Mtera 80 MW
- Hale (Tanga) 68 MW
- Rusumo 80 MW
- Julius Nyerere 2,115 MW
- Nyumba ya Mungu 8 MW
Kwa hiyo, kupitia vyanzo vya maji tuna uwezo wa kuzalisha 2,735 MW. Mahitaji ya umeme nchini yanakadiriwa kuwa 2,200 MW. Hii ina maana kwamba tuna ziada ya karibu 500 MW ambazo tunaweza kuuza nje. Kwa hiyo hatujadanganywa. Umeme wa kuuza nje upo.
Sasa, kwanini tununue umeme nje wakati ndani tuna ziada? Jibu ni kwamba usafirishaji wa umeme unasababisha upotevu njiani. Kusafirisha umeme si sawa na kusafirisha mbaazi. Ukitoa mbaazi Moshi zikiwa 50Kgs, zikifika Dar zitakua hizohizo 50Kgs. Lakini kwa Umeme ni tofauti. Kadri unavyosafirisha umbali mrefu, ndivyo unavyopotea.
Je, kati ya Ethiopia na bwawa la Mwalimu Nyerere, wapi mbali? Kama tunahofia umeme ukisafirishwa kutoka bwawa la Nyerere hadi Arusha utapotea, je unaotoka Ethiopia si utapotea zaidi?
Jibu ni kwamba Tanzania haitahusika na usafirishaji wa umeme huo kutoka Ethiopia. Sisi tutahusika baada ya kuupokea Namanga. Kwa hiyo, kama ni usafirishaji, sisi tutaanzia Namanga kwenda Arusha. Kwahiyo pale Namanga tukipokea 100MWs tutazifikisha Arusha bila kupotea maana ni karibu.
Kwa lugha rahisi, ni sawa na kuwa na chanzo kipya cha umeme Namanga. Kwa hiyo ni ukweli kwamba kusafirisha umeme kutoka Namanga kwenda Arusha hakutakuwa na upotevu mkubwa njiani kama kusafirisha umeme kutoka bwawa la Nyerere kwenda Arusha. Hii ni logic ya kawaida ambayo hata mtoto mdogo anaelewa.
Ili tuweze kusafirisha umeme kutoka bwawa la Nyerere au Mtera hadi Arusha bila kupotea sana, inabidi tujenge vituo vya kupoozea njiani (substations) kama ile ya Lemuguru iliyopo Mateves Arusha, ambayo ilianza kujengwa 2019 imekamilika 2024 (miaka mitano) kwa gharama ya karibu bilioni 20. Kwa hiyo kuna suala la muda na gharama.
Je, umeme wa ziada unaozalishwa Tanzania utaenda wapi? Jibu ni kwamba Utauzwa nje ya nchi. Tayari Tanzania imesaini hati ya makubaliano (MoU) na Zambia na Rwanda kuziuzia umeme.
Je, kusafirisha umeme kwenda nchi hizo hakutafanya upotee njiani? Jibu ni kwamba umeme huo utauzwa kutoka vyanzo vya karibu, hivyo hakutakuwa na upotevu mkubwa. Kwa mfano, Rwanda watauziwa umeme kutoka Rusumo na Zambia watapokea umeme kutoka Kihansi ambapo upotevu hauwezi kuwa mkubwa kama kuutoa umeme Kihansi kwenda Arusha au Rusumo kwenda Arusha.
Utaratibu wa kuuziana umeme baina ya nchi na nchi sio jambo geni. Nchi za Afrika Mashariki zimeanzisha Eastern Africa Power Pool (EAPP) ili kuratibu biashara ya umeme na uunganishaji wa gridi kati ya nchi hizo.
Nchi za Ulaya wanayo European Network of Transmission System Operators for Electricity (ENTSO-E) ambayo inaunganisha nchi 35 za Ulaya. Kupitia ENTSO-E nchi inaweza kuuza na kununua umeme kutoka nchi jirani. Kwa mfano, Ujerumani inanunua umeme kutoka Ufaransa, Denmark, na Norway jumla ya 30,000 MW. Lakini Ujerumani hiyohiyo inauza umeme kwa Ufaransa, Austria, na Uholanzi ambao ni 60,000 MW.
Unaweza kujiuliza, kama Ujerumani inaweza kuzalisha umeme na kuuza nje ya nchi, kwanini tena inunue? Jibu ni kwamba inapunguza upotevu wa kusafirisha umeme kwa umbali mrefu ndani ya nchi. Kuliko kutoa umeme Munich na kuusafirisha hadi Humburg (kilomita karibu 800) ni bora wakanunua umeme Dernmark wakapeleka Humburg, halafu ule wanaozalisha Munich ukatumika miji ya jirani na mwingine wakauzia Austria.
Na Tanzania ndicho tulichofanya. Kuliko kutoa umeme Rusumo kuupeleka Kyela, ni bora ule wa Rusumo utumike Kigoma, Kagera, na Geita, halafu unaobaki tuwauzie Rwanda na Burundi. Halafu tununue umeme kutoka Malawi tupeleke Kyela. Tukifanya hivyo tutakua tumeokoa gharama za usafirishaji na upotevu wa umeme njiani.!
0 Comments