Header Ads Widget

JIMBO LA NZEGA VIJIJINI SEHEMU YA KWANZA


Leo tunaingia rasmi jimbo la Nzega vijijini katika kuangazia na kuchambua mambo kadhaa yanayohusiana na maendeleo ya kisiasa na kiuchumi kwa ujumla wake.

Tutaeleza pia ni kwa nini majimbo haya mawili, Nzega Vijijini na Bukene yamekuwa yakikimbiliwa sana na wanasiasa wengi wanaotaka ubunge.

Kabla hatujaingia kiundani juu ya mambo hayo ningependa kueleza historia (chimbuko) la jimbo hili la Nzega vijijini  na Mbunge aliyepo ambaye ni Dkt. Hamis Kigwangalla, tangu jimbo la Nzega halijagawanywa kuwa majimbo mawili (Nzega Mjini na Nzega vijijini).

Mbunge wa Nzega Vijijini Dkt. Hamisi Kigwangalla 


Nianze na hili la ubunge, Dkt Hamis Kigwangalla amekuwa Mbunge tangu 2010 akipokea kijiti kutoka kwa Mzee Lucas Lumambo Selelii wakati huo likiitwa Jimbo la Nzega.

Ujio wa Dkt. Kigwangalla ulipokewa kwa nderemo na vifijo na wapenda mabadiliko wote, wakiamini mkombozi (Musa) waliyemsubiri tangu - kaja ili awavushe kuelekea nchi ya ahadi (Nzega ya neema).

Pamoja na matumaini hayo ya wapenda mabadiliko, lakani mabadiliko hayo hayakupatikana kama walivyokusudia kutokona na ukweli kwamba Dkt. Kigwangalla alipitia dhoruba kali sana ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiasi kwamba kama angekuwa mtu mwingine angeomba kujiuzulu ubunge na kuachana na siasa kabisa.



Kwanza alitengwa na karibu viongozi wote wa CCM, na alitengwa si kwa sababu alikuwa mbaya, ila ni kutokana na mshindani wake wa 2010 Hussein Bashe ambaye alikatwa jina lake kwa sababu ni Msomali, yaani hakuwa raia wa Tanzania, na upo uwezekano mpaka sasa haijulikani uraia wake na haujaelezwa ikiwa process za kuwa raia zilikamilika.

Huyu bwana Hussein Bashe aliletwa Nzega kugombea ubunge na akina Lowasa na Lostam baada ya aliyekuwa Mbunge wa Nzega, Mzee Lucas Selelii kuonekana amewasaliti akina Lowasa na kujiunga na wazalendo akina Samwel Sitta na Mwakyembe wakati wa sakata la Richmond.

Ikumbukwe kuwa Mbunge Selelii aliteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya Dk. Mwakyembe ya kufuatilia Richmond, na katika team hiyo wao Selelii na Mwakyembe walioonekana vinara wa kulivalia njuga sana suala la Richmond.

Ndipo vita ikapamba moto baina ya Mbunge Selelii na Mbunge Dk. Mwakyembe, sote tunakumbuka jinsi Dk. Mwakyembe alivyonusulika kifo kwa kutegewa sumu Hotelini.

Kwa upande wa Mbunge Selelii, pamoja na kwamba aliweza kuvuka vihunsi vya sumu, lakini bado alikutana na kikwazo kwenye uchaguzi wa 2010, kwani aliletwa Hussein Bashe ili kumng'oa Selelii kwa gharama yoyote.

Kwa hiyo zilimwagwa fedha nyingi sana za kuhonga wapiga kura ambazo zililetwa na wakala Sofia Simba kutoka mafisadi hao, na hapo ndipo zilipoanzia siasa za maji taka hapa Nzega.

Kutokana na vita hiyo ya kisiasa kuwa kali, kamati na Halmashauri kuu NEC, chini ya Mwenyekiti Jakaya Kikwete ikaamua kurudisha jina la Dkt. Hamis Kigwangalla.

Vita ikahamia kwa Dkt. Kigwangalla, kwani naye alikumbana na changamoto nyingi kwenye ubunge wake ambazo bila shaka mpaka leo zimemwandama.


Dkt Hamis Kigwangalla alishinda uchaguzi mkuu wa 2010 kupitia kuungwa mkono zaidi na vyama vya upinzani ulioushawishi umma kutokana na kumkubali kwake wananchi. Asilimia 90 ya wana CCM walihamasishwa na viongozi wasimuungue mkono Dk. Kigwangalla.

Na hata aliposhinda uchaguzi bado viongozi wa CCM waliwazuia wanachama kumuunga mkono Dkt. Kigwangalla kwenye shughuli zake za kibunge.

Haya ndiyo madhira aliyoyapitia Dkt. Kigwangalla kwenye ubunge wake wa kwanza wa miaka mitano.

Kwa nini Dkt. Kigwangalla alionekana mkombozi wa wana Nzega?

Ni kwa sababu Dkt. Kigwangalla anafahamika kama mtu machachari tangu ujana wake, na hulka yake hii ilijitokeza na kuvuma zaidi wakati ule akiwa Rais wa Madaktari Tanzania, pale Mhimbili alipoanzisha maanamano ya mgomo wa madaktari.

Hulka ya Dk. Kigwangalla ni ya kiwanamapinduzi, yeye ni mwanaharakati aliyetengenezwa na historia ya maisha yake kuanzia ngazi ya familia, ngazi ya jamii na taasisi za elimu alimopita. 

Kwa hivo ana chembechembe za kiuanamapinduzi.

Shujaa au Jambazi hawaibuki tu hivi hivi, bali hutangenezwa na jamii anamokulia shujaaa au jambazi huyo.

Hii ndiyo iliwapa urahisi wapenda mabadiliko na kuamini kuwa mkombozi wao kaja.

Na haya ifahamike siyaelezi kwa ushabiki, mimi sijawahi kuwa mshabiki kwenye mambo ya msingi, nayaeleza haya kama mwanazuoni.

Wanazuoni hutofautishwa na wasomi au watu wengine kwa sifa kuu zifuatazo:

Moja ni kwamba mwanazuoni huchambua mambo kihistoria. Tukio au jambo limetoka wapi, liko wapi na linaelekea wapi. Mwongozo wake ni kuchambua mwelekeo na ndicho ninachokifanya hapa.

Pili, mwanazuoni huamini kwamba ukweli haugawanyiki, maana yake ni kwamba huwezi kupata ukweli wa jambo kama hujaliangalia jambo hilo katika muktadha wake.

Tatu, mwanazuoni ni wakala wa mabadiliko ya hali iliyopo, na siyo mtumwa wake. Dhamira yake ni kuleta hali bora katika jamii, hususan kwa walio wengi.

Yeye daima ni mpambanaji, anapambana dhidi ya dhuluma, uonevu, ukandamizaji na uovu mwingine popote ulipo.

Ndiyo dhamira yake, ndiyo maisha yake, na ndiyo uhai wake. Anajitambulisha na wapambanaji wenzake bila kujali wanakotoka, itikadi, dini, makabila yao, au rangi yao.

Nne, mwanazuoni hujali, na kupigania maendeleo ya wanadamu, maendeleo ya wote, siyo ya wachache.

"Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko". ni moja ya imani yetu ya CCM.

Nimeyagusia haya kwa lengo la kuupa umma uelewa, ili usije kupotoshwa na wasiopenda ukweli na uwazi, wanaonufaika na ufisadi, dhuluma, uongo,  unyanyasaji na hata uovu. Hivyo, haya ninayoyajadili hapa ni kwa maslahi ya jamii na wapenda mabadiliko wote.

Binafsi sijawahi kufanya kazi na Dkt. Kigwangalla, wala hajawahi kunipa kazi yake yoyote ya kisiasa niifanye. Dk. Kigwangalla ni mtu ambaye aliingia kwenye ubunge na wengi tulimkubali kwa falsafa yake ya uongozi.

Kama binadamu anaweza kuwa na mapungufu fulani fulani, hayo yanapatikana pia kwa binadamu wengine, yale mapungufu ya kisiasa tutayasema na hilo ni haki yetu na ni haki yake kusemwa maana yeye siyo kama mitume wa mwenyezi Mungu ambao hawapaswi kupingwa wala kukosolewa na wafuasi wao.

Wakati akiwa mbunge wa jimbo la Nzega, mimi nilikuwa katibu wa UVCCM kata ya Nzega Mjini Mashariki, nilipinga ubaguzi wa viongozi wa CCM uliofanywa dhidi ya mbunge huyu wa kutompa ushirikiano, vijana wote wa CCM niliwaeleza juu ya madhara ya kutumika vibaya na wanasiasa, badala yake tukawataka wafanye kazi ya CCM kila inapobidi, kisha ndiyo waende kwenye makundi yao bila kuathiri kazi za chama.

Vijana walituelewa na ikawafanya hata wale vijana waliokuwa team Bashe waungane nasisi kwani ubaguzi wao haukuwasaidia chochote, maana ilikuwa wasipoungana nasi ni kama wameungana nasisi, wakaona isiwe tabu wakubali kufanya kazi za CCM.

Na kwa kufanya hivyo jumuiya ya UVCCM Nzega ilionekana kuwa na nguvu kubwa sana katika Mkoa wa Tabora.

Kwa hiyo, baada tu ya kuwa mbunge wa jimbo la Nzega, Dkt. Kigwangalla hakuchelewa akanza kupambana na ufisadi, aliongoza maandamano ya wananchi kuelekea kwenye mgodi wa Nzega kwenda kudai haki ya wananchi.

Kwa kuwa Bashe alikuwa amewashika viongozi wa chama na serikali kuanzia Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Mkurigenzi na wakuu wa idara, kazi ya hawa viongozi ikawa kama ya remorti, walielekezwa kila kitu cha kufanya, Mbunge Dk Kigwangalla alipigwa mabomu na polisi, wakachezea stiki pamoja na wananchi wake na kuwekwa ndani.



Baada ya Mbunge kuikomboa fedha iliyokuwa ikidaiwa pele mgodini, alishauri na kupendekeza fedha hiyo ikanunue mitambo ya kuchimba visima na ya kuchonga barabara, lakini pia fedha ambayo ingebaki ifunguliwe SACCOS ya wananchi ili kusaidia wajasiriamali wadogo wadogo (vijana, kina mama na walemavu).

Lakini bado alipigwa vita na madiwani waliotumika na Bashe, ambao yeye Dkt. Kigwangalla aliwaita "Madiwani mizigo ya mavi", kwani pesa hiyo badala ya kununua hiyo mitambo, ilipofika tu Halmashauri Madiwani wakaielekeza iende kujenga maabara shuleni, jambo ambalo halikutekelezwa mpaka leo, wakaifisadi fedha hiyo ambayo hapo mwanzo walimpinga Kigwangalla aifanikiwe kuikomboa.

Haya ni moja tu ya mambo ambayo yalimkatisha tamaa Dkt. Kigwangalla na asiweze kuibadili jamii ya wana Nzega, tangu hapo hana hamu tena na watu wa Nzega, nitakuwa muongo kama nitakuwa bado naamini kuwa Dk. Kigwangalla bado anayo dhamira ya kuleta mabadiliko katika jimbo la Nzega vijijini na Nzega kwa ujumla.

Tangu alipoona viongozi wa CCM, hata wale wa kuchaguliwa kwenye kata na matawi ambao ndio walipaswa kuwa sehemu ya harakati na mapambano ya kuleta mabadiliko, wakaendelea kuungana na msomali kuhujumu maendeleo ya wananchi, hapo ndipo Kigwangalla akalazimika kuingia katika siasa za hovyo, za kutafuta ushindi tu bila kujali anashinda kwa njia gani.

Hoja ya kwa nini wanasiasa wengi wanakimbilia sana majimbo ya Nzega vijijini na jimbo la Bukene, hili nitalieleza zaidi kwenye makala ya pili ijayo...

Kwiyeya Singu. 0784977072

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI