RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi anatarajia kufungua Tamasha la Tatu la Uwekezaji Zanzibar linalorajia kufanyika Mei 07 na 08 mwaka huu Micheweni Pemba.
Tamasha hilo litahusisha Wawekezaji wa Ndani na Nje ya Nchi, Viongozi wa Wafanyabiashara, Taasisi za Umma na Binafsi.
Akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Shariff Ali Sharif amesema kuwa, Tamasha hilo ni kichocheo cha mabadiliko ya kiuchumi na kuweka Pemba kuwa kituo cha Uwekezaji wa Kimataifa.
Amesema lengo kuu la Tamasha hilo ni kuitangaza Pemba kuwa kisiwa cha kuvutia Uwekezaji katika madhari ya uchumi wa Zanzibar.
Amefahamisha kuwa kwa sasa Pemba ina fursa kubwa ya Uwekezaji hivyo Serikali imejidhatiti kuhakikisha wanaweka mazingira bora na kuwavutia Wawekezaji kuwekeza kisiwani Pemba na kufungua fursa nyingi za ajira kwa vijana.
"Tamasha hili linaashiria mwanzo wa enzi mpya ya upanuzi wa kiuchumi na kuonesha fursa kubwa za zilizopo kisiwani Pemba katika Sekta mbalimbali na kuchangia ongezeko la ajira na kuboresha maisha ya waakazi wake," ameeleza.
"Katika Tamasha hili kutakuwa na jukwaa litakalo weka mkakati wa wa kupata fursa za ushirikiano wa moja kwa moja kati ya Wawekezaji, Viongozi wa Biashara na taasisi za Serikali na Binafsi," amefafanua
Aidha ameeleza kuwa, Kutakuwa na Mjadala ambao utaangazia mifumo ya Sera na mikakati inayolenga kuboresha urahisi wa kufanyabiashara Zanzibar pamoja na kukuza maendeleo jumuishi.
Amefafanua kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara yanayoyanufaisha Wawekezaji na Wananchi kwa Ujumla.
0 Comments