Header Ads Widget

CHANZO CHA UKATILI,UJAMBAZI KAMBI ZA WAKIMBIZI CHABAINISHWA

Baadhi ya wakimbizi wa Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wanaohifadhiwa kwenye kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu wilayani Kasulu mkoani Kigoma wakiwa kwenye maandamo ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika kambini hapo
Mwenyekiti wa kamati ya wanawake katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma Butunga Salange akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika kambini hapo
Mkurugenzi wa idara ya wakimbizi ya wizara ya mambo ya ndani ya nchi Sudi Mwakibasi akizungumza na wakimbizi wa Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wanaohifadhiwa katika kambi ya wakimbi ya Nyarugusu wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika kambini hapo

Na Fadhili Abdallah

MKURUGENZI wa idara ya huduma za wakimbizi ya wizara ya mambo ya ndani ya nchi Sudi Mwakibasi amesema kuwa kitendo cha wazazi na walezi kusimamia zaidi malezi na matunzo kwa watoto wa kike na kuwaacha wa kiume wakijilea wenyewe ndiyo chanzo kikubwa cha vitendo vya ukatili, ujambazi na mambo yasiyofaa yanayofanywa na wanaume kwenye kambi za wakimbizi nchini.

Mwakibasi alisema hayo katika maadhimisho ya siku ya wanawake dunia yaliyofanyika kwenye kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma ambapo alisema kuwa watoto wa kike tangu wanapokwa wadogo wameweka taratibu za malezi za ulinzi na matunzo huku watoto wa kiume wakiachwa wafanye wanavyoona wao.

Kutokana na hilo Mwakibasi alisema kuwa imefanya watoto wengi wakiume kuingia kwenye makundi hatari ikiwemo masuala ya ujambazi, kurubuniwa na kurudi kwenye mapigano kwenye nchi zao na nchi nyingine lakini pia imesababisha watoto hao wa kiume kufanya vitendo vya ukatili ikiwemo ukabaji na ulawiti.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Mratibu anayehusika na kitengo cha masuala ya jinsia na kupinga ukatili kutoka Shirika la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), Rehema Katega alisema kuwa wasichana na wanawake kwenye makambi ya wakimbizi wanahitaji haki na usawa ikiwemo kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.

 Mwenyekiti wa kamati ya wanawake katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma,Butunga Salange alisema kuwa changamoto kubwa ni wanaume kuwatelekeza na kuwakimbia wanawake zao zao hivyo kuwaacha wanawake hao na mzigo mkubwa wa malezi ya watoto.

Alisema kuwa kutokana na hali hiyo inawawia vigumu kwenye malezi na kutokana na hali ya kambi wamekuwa wakiweka jitihada kubwa kwenye matunzo na ulinzi wa watoto wa kike wasipate madhara ukilinganisha na watoto wa kiume.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI