Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WAENDESHA pikipiki za abiria maarufu kama bodaboda wanaelezwa kuwa changamoto kubwa katika suala la kudhibiti ajali za barabarani hasa kwenye vivuko vya watembea kwa miguu kutokana na kutozingatia sheria za usalama na hivyo kusababisha ajali nyingi kwa watoto na wanafunzi.
Mkuu wa kituo cha kikanda cha umahiri katika usalama barabarani kanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, Godlisten Msumanje alisema hayo wakati wa mafunzo kwa wanafunzi wa shule za msingi wilayani Kasulu kuhusu taratibu za kuzingatia usalama barabarani ikiwa ni sehemu ya mradi wa barabara ya kiwango cha lami Kutoka Manyovu wilaya ya Buhigwe kupitia Kasulu Hadi Kabingo wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma.
Msumanje alisema kuwa uwepo wa barabara nzuri unafanya vyombo vya moto kwenda kwa kasi hivyo kumekuwa na madhara makubwa kwa watu na mali zao na kwa wanafunzi hivyo mradi huo unatoa elimu kupitia chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa makundi mbalimbali ikiwemo bodaboda ili uwepo wa barabara hizo uwe na tija kiuchumi na kupunguza madhara ya ajali kwa wananchi.
Alisema kuwa kwa sasa bodaboda zimekuwa nyingi kuliko magari na ndizo ambazo hata maeneo ya vivuko madereva wake licha ya kujua sheria za usalama barabarani lakini wamekuwa hawazingatii sheria na hivyo kuathiri wanaotembea kwa miguu.
Akizungumza katika mafunzo hayo Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Mazoezi Kiganamo wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Anold Ndolele alisema kuwa bodaboda imekuwa tatizo kubwa ambalo linaathiri watembea kwa miguu wakiwemo wanafunzi wakati wa kuvuka barabara na hali hiyo imekuwa na athari hata kwa shule yao ambayo iko pembezoni mwa barabara kuu ya lami ya Kasulu kwenda Kibondo.
Kutokana na hali hiyo ambayo imesababisha kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wanafunzi wao ikiwemo kuwapeleka Kigoma mjini kujifunza kwenye maeneo ya vivuko, taa za barabarani alama nyinginezo jambo ambalo limesaidia kupunguza ajali kwa wanafunzi wa shule hiyo.
0 Comments