Header Ads Widget

WAZIRI KIKWETE AVALIA NJUGA UJENZI WA BARABARA YA MBALIZI - MKWAJUNI HADI MAKONGOLOSI.



Na Moses Ng'wat, Songwe.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwan Kikwete, ameahidi kufuatilia kwa ukaribu mchakato wa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mbalizi - Mkwajuni hadi Makongolosi yenye urefu wa kilometa 128, akitambua umuhimu wake kwa uchumi na maisha ya wakazi wa Songwe na mikoa jirani.


Akizungumza leo Februari 24, 2025, mara baada ya kukagua ujenzi wa madarasa sita katika shule ya sekondari Kanga, akiwa katika  ziara yake wilayani Songwe, Kikwete, ambaye pia ni mlezi wa mkoa huo, alisema barabara hiyo ni kiunganishi muhimu cha mikoa ya  Nyanda za Juu Kusini na mikoa ya Kati, ikiwemo ile ya Kanda ya Ziwa, hivyo ni lazima iharakishwe ili kurahisisha usafiri na kuchochea biashara.

"Badala ya watu wanaotoka Mbeya au Songwe kulazimika kuzunguka hadi Iringa kwenda Singida, barabara hii ikikamilika itarahisisha safari kwa kuwa watu watakatiza hapa hadi Makongolosi na kuelekea mikoa mingine ya Kati na Kanda ya Ziwa," alisema Kikwete.

Aliongeza kuwa mkandarasi wa mradi huo ameshapatikana na tayari mazungumzo yamefanyika, huku akiahidi kuwa ndani ya mwezi mmoja, mkandarasi ataanza kuleta vifaa na kazi itaanza rasmi ifikapo Juni mwaka huu.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe, Mhandisi Joseph Mayaya, alieleza kuwa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 128 itaanza kwa awamu ya kwanza kwa kujengwa kilometa 10 kwa kila mkoa, yaani Songwe na Mbeya.


Akisoma taarifa ya Wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Solomon Itunda, alisema wilaya hiyo imeendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato, ambapo matarajio ni kukusanya shilingi bilioni 4.6 katika mwaka huu wa fedha.

Alibainisha kuwa sekta ya afya imenufaika kwa kupokea shilingi bilioni 12, huku sekta ya barabara ikipatiwa shilingi bilioni 9 ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. 

Alisema kwa upande wa TARURA Wilaya hiyo imepokea shilingi bilioni 8 kwa ajili ya ujenzi wa mtandao wa barabara za lami katika mji wa Mkwajuni, makao makuu ya wilaya hiyo.

Kwa upande wake , Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Cecilia Kavishe, alisema  Halmashauri ilipokea kiasi cha shilingi milioni 150 kwa ajili ujenzi wa madarasa hayo kwa lengo la kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule hiyo ya Kanga yenye jumla ya wanafunzi 1200 wa kudato cha kwanza hadi sita.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Songwe, Radwell Mwampashi, alimweleza Kikwete kuwa hali ya kisiasa mkoani humo iko shwari, huku viongozi wa serikali na chama wakishirikiana kuhakikisha maendeleo kwa wananchi.


Katika ziara yake ya siku tatu mkoani Songwe, Kikwete pia anatarajiwa kukagua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 700, ikihusisha sekta za elimu, afya, na miundombinu.

Miongoni mwa miradi hiyo ni Kituo cha Vijana cha Sasanda wilayani Mbozi, ambapo atakagua shamba la vijana katika kituo hicho.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI