Header Ads Widget

WAWILI WAMEFARIKI KWA KUANGUKIWA NA KIFUSI


Na Lubango Mashauri, Matuko Daima App.

WATU Wawili waliofahamika kwa Majina ya Jeradi Mathias mkazi wa Kakola Wilayani Kahama na Mussa Stivin Kinyami mkazi wa Masumbwe wilayani Kahama ambao ni wachimbaji wa madini ya dhahabu wamefariki dunia baada ya kuangukiwa na kifusi wakiwa ndani ya duara katika mgodi namba sita uliopo Kata ya Igurubi Tarafa ya Igurubi Wilayani Igunga Mkoani Tabora. 

Wakizungumza kwa simanzi na majonzi baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa, walipata taarifa tarehe 25.02.2025 majira ya saa mbili asubuhi kuwa kuna watu wamefukiwa na kifusi wakiwa ndani ya duara katika mgodi namba sita kijijini hapo. 

"Kama mnavyoona wenzetu wamepata ajali toka jana (juzi) tarehe 25.02.2025 majira ya saa mbili asubuhi na juhudi za kuwaokoa ziliendelea mpaka usiku jana (juzi) na leo asubuhi hii kama mnavyoona tumefanikiwa kuutoa mwili mmoja majira ya saa 12 asubuhi ya leo tarehe 26.02.2027 tunaendelea na zoezi la kuhakikisha na huyo mmoja aliyesalia ndani ya kifusi tumuokoe, " alisema Daud Allan.

Aliendelea kusema kuwa, " Changamoto ni kuwa lililetwa skaveta kwa ajili ya uokoaji lakini kutokana na ardhi kutitia kutokana na uzito wa skaveta limesitishwa hivyo tunaendelea kwa kutumia njia ya kawaida ya kufukua chini na kupandisha udongo juu kwa kutumia mashine na madumu. "

Huku Patrick Mdadila mkaguzi kutoka kampuni ya Kasala Mining akisema kuwa udongo ambao umekuwa ukititia ni kikwazo kwao na kufanya zoezi hilo kuchukua muda mrefu.

" Mimi ni jirani na mgodi huu tulipopata taarifa tumefika na kukuta zoezi la uokoaji likiendelea, tumeumia sana kwani matukio kama haya yanapotokea hata sisi wachimbaji wengine tunaingiwa na hofu," akisema Paul fabian.

Kwa upande wake Katibu wa Wachimbaji madini Igunga William John akibainisha kuwa kuna baadhi ya watu ambao wanafika katika migodi na kuto kuandika majina yao halisi, mahali wanakotoka na mawasiliano ya ndugu zao, hali ambayo itasaidia kujua ni wapi mtu anapo pata taizo kwa kumpeleka.

"Hivi karibuni tutaitisha kikao na wachimbaji wote na kuwaeleza kuwa ili mtu aingie kufanya kazi katika migodi lazima awe na kitambulisho cha NIDA, majina ya ndugu zake na mawasiliano, kwani ofisa mkazi wa madini ametuambia kila mtu afahamu anakotoka ndio tupompokee, hii itasaidia kupunguza vifo vya kizemba vya ndugu zetu, " alisema William John.

Mmiliki wa Mgodi huo namba sita, Daud Mwita alipoulizwa na Waandishi wa Habari juu ya tukio hilo alisema hajui chochote kinachoendela hivyo atafutwe meneja wake wa mgodi kwani yeye ndiye anajua kila kitu juu ya tukio hilo na amemkasimisha majukumu yote ya utendaji kazi.

" Mimi ni mgeni kama wewe ndio maana nimesema sifahamu, ila taarifa ya kusimamisha mgodi niliipata mimi nikawamabia waniandikie kwa barua wakaniambia nifanye maelekezo nikawaambia mbona sijapata barua ya marekebisho mnakuja tu kufunga mgodi wakaniambia wamempatia meneja wangu na nifukie mashimo yote, " alisema Daudi Mwita na kuongeza kuwa, 

" baada ya kufukia mashimo yote walikuja na kujiridhisha na kuniandikia barua nianze kazi baada ya kufuata maelekezo yao hivyo tukio hili lilipotokea mimi sikuwepo nilipatiwa taarifa tu. "

Naye Meneja wa mgodi huo namba Sita Emmanuel Lemigius amesema wakati watu hao wanaingia shimoni hakuwepo hivyo alipatiwa taarifa juu ya watu hao kufukiwa na kifusi ambao ni Mussa Stivin Kinyami na Jerad Mathias.

" Chanzo cha ajali hii ni kifusi, kwani waliingia ndani ya duara kufanya tathimini ya kurekebisha eneo lililo bovu ambalo walikusudia kulifanyia kazi, kwa hiyo walipokuwa chini kwenye system kufanya tathimini ndio udongo ukashuka,"

" Eneo lilikuwa ni salama kwani tulipewa barua na RMO tufanye lakini sikumbuki ni lini alinipatia barua hiyo ya kuanza kazi, hivyo ni mazingira tu ya ajali kama ulivyo yaona, kwani tulipewa barua ya kufungiwa kwa njia ya Whatsapp na hata ya kufunguliwa mgodi sijui maana sikumbiki ila walifika wenyewe wakiwa na meneja Frenk, kyanabo, injinia wa madini  na ofisa madini aitwaye  Gasper. "

Fatuma Kyando ni ofisa madini mkoa wa Tabora amesema kuwa waliufungia mgodi huo tarehe 7.01.2025 na kuufungulia tarehe 16.01.2025 baada ya kuwapatia maelekezo wamiliki wa mgodi huo ikiwa ni kufukia maduara yote ambayo hayatumiki na kurekebisha maduara ambayo yanatumika. 

" Nakumbuka wakati nafunga niliwapa maelekezo ya vitu vya kifanya na moja wapo ni kufukia maduara yote ambayo hayafanyi kazi na maduara ambayo yanafanya kazi wayaimarishe ikiwa ni kufunga yale matimba (miti) kuwa imara zaidi na matimba yawe ya uhakika ili kuimalisha usalama kwa watu wao, " akisema Fatuma Kyando. 

Akithibitisha kupokea miili hiyo Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Igurubi Maridadi Mwagala amesema kuwa " leo tarehe 26.02. 2025 tumepokea miili ya wachimbaji wawili ambao walipata ajali kule machomboni namba sita na tumeifanyia uchunguzi na tumeihifadhi katika chumba cha kuhifadhi maiti kwa ajili ya mazishi."

Mwenyekiti wa CCM kata ya Igurubi Kisena Ikobya, ametoa wito kwa wachimbaji na viongozi wa migodi kujiimalisha katika machimbo yao na kufuata sheria za uchimbaji. 

Akitoa Salamu za Pole kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo, Afisa Tarafa ya Igurubi Judith Haule amewashukuru wananchi na viongozi wote waliojitokeza na kushiriki katika zoezi hilo la uokoaji ambapo kwa bahati mbaya watu hao wameokolewa tayari wakiwa wamefariki.






Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI