WIZARA ya Katiba na Sheria imewataka wadau na watoa huduma za msaada wa kisheria kufuata kanuni zinazowaongoza na kuwa mstari wa mbele katika kutatua migogoro ya kisheria ngazi ya jamii.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt, Franklin Rwezimula, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku kumi na tano kwa watoa huduma za msaada wa kisheria kwa niaba ya Katibu Mkuu Eliakim Maswi.
Dkt, Rwezimula amesisitiza kuwa jukumu la wasaidizi hawa ni muhimu sana katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii na kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa watu wote, bila kujali hali zao za kiuchumi au kijamii.
Amesema kuwa ni muhimu kwa watoa huduma hawa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kuimarisha amani katika Rwezimula
" Nisisitiza kwamba wasaidizi wa kisheria wanapaswa kuwa mfano bora wa kuigwa katika uhamasishaji wa masuala ya kisheria niwataka washiriki kutumia mafunzo haya kama fursa ya kujifunza na kuimarisha uwezo wao katika kutatua matatizo ya kisheria kwa njia ya amani na ya ushirikiano," Amesema Dkt Rwezimula
Kwa upande wake Mwakilishi wa shirika la LSF, Aman Manyalezi, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia kanuni na taratibu katika utoaji wa msaada wa kisheria huku akiwataka wadau wote wanapaswa kushirikiana ili kuboresha huduma na kufikia wanajamii wengi zaidi.
"Niwakumvushe wenzangu katika mafunzo haya pia umuhimu wa kutoa elimu ya sheria kwa jamii ili kujenga uelewa wa pamoja na kusaidia kupunguza migogoro ya kisheria, " Amesema
Naye Mshiriki wa mafunzo kutoka Mbulu, Monica Mathias, ameeleza matumaini yake ya kuboresha uwezo katika kutatua migogoro ya kijamii. Amesema mafunzo haya yamejenga uelewa mkubwa kuhusu masuala ya kisheria na kuwasaidia wahanga.
"Ningependa kupendekeza kuanzishwa kwa vikundi vya msaada wa kisheria katika maeneo yetu ili kuongeza ufanisi," amesisitiza.
Kwa upande wake, Juma Waziri, mshiriki kutoka Tanga, amesema mafunzo haya ni hatua muhimu katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wanajamii wengi huku akisisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo watoa huduma ili waweze kutoa msaada wa haraka na wenye ufanisi.
" Niwazi kuwa mafunzo haya yatasaidia kupunguza idadi ya kesi zinazofikishwa mahakamani, hivyo kuimarisha mfumo wa haki," amesema.
Hata hivyo Washiriki zaidi ya arobaini kutoka mikoa mbalimbali wanapata mafunzo haya ya kujengewa uwezo, ambapo lengo ni kuwasaidia kushughulikia mashauri kabla ya kufikishwa mahakamani na hii ni njia muhimu ya kuboresha mfumo wa haki na kuimarisha uelewa wa sheria katika jamii pia Mafunzo haya yanatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika utoaji wa huduma za kisheria, hivyo kuwezesha jamii kuwa na uelewa mzuri na uwezo wa kujitetea katika masuala yao ya kisheria.
Mwisho
0 Comments