Na Hamida Ramadhan Matukio Daima App Dodoma
WATAALAM kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) wamefanikiwa kuvuka mipaka ya nchi na kwenda kutoa huduma za matibabu ya moyo katika nchi jirani zikiwemo za Malawi, Zambia na Jamhuri ya Watu wa Comoro.
Hayo yamesemwa leo jijini hapa na Peter Kisenge Mkurugenzi Mtendaji
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete wakatia akiongea na waandishi juu ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka Minne ya uongozi w serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan
Amesema kuwa,wakiwa katika nchi hizo walitibu wagonjwa 1,189 watu wazima walikuwa 851 na watoto 338 huku Wagonjwa 262 walipewa rufaa ya kuja kutibiwa JKCI.
Ameeleza kuwa Wagonjwa waliotibiwa kutoka nje ya nchi walikuwa 689 Wagonjwa hao walitoka katika nchi za Somalia, Malawi, Kenya, Rwanda, Jamhuri ya Watu wa Comoro , Msumbiji, Nigeria, Siera Leone, Zimbabwe, Zambia, Uganda, Congo, Ethiopia, Burundi na wengine kutoka nje ya Afrika zikiwemo nchi za Armenia, China, Ujerumani, India, Norway, Ufaransa na Uingereza.
"Wagonjwa waliofanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua na kubadilishwa Valvu za moyo moja hadi tatu, upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu ya moyo (Coronary Artery Bypass Graft Surgery —CABG), upasuaji wa mishipa ya damu na mapafu walikuwa 2,784 kati ya hao watu wazima walikuwa 1,880 na watoto 904," Amesema.
Na kuongeza "Upasuaji mpya wa moyo wa kufungua kifua uliofanyika ni wa kurekebisha mshipa mkubwa wa damu uliotanuka kwenye kifua na tumbo, kurekebisha valvu za moyo kwa watu wazima, kurekebisha mshipa uliotanuka kwenye bega, kupandikiza mishipa ya damu wakati moyo unafanya kazi bila ya kuusimamisha, kukarabati mlango wa moyo wa mshipa mkubwa wa damu iendayo kwenye mapafu kwa kutumia chumba cha moyo cha juu kulia, kutoa dawa ya kuzuia maumivu sehemu ya uti wa mgongo wakati wa upasuaji mkubwa wa moyo, "Amesema
Amesema Kupitia mtambo wa Cathlab (Catheterization Laboratory) ambao ni maabara ya uchunguzi wa matatizo na tiba ya magonjwa ya moyo inayotumia mionzi maalum wagonjwa 8,789 walipata huduma ya matibabu kati yao watu wazima walikuwa 7,997 na watoto 792. Wagonjwa hawa walipata huduma za uchunguzi, matibabu ya mishipa ya damu ya moyo iliyokuwa imeziba na kuwekewa vifaa visaidizi vya moyo.
Amesema Wagonjwa 469 walitibiwa tatizo la mfumo wa umeme wa moyo kwa kutumia mtambo wa kawaida na 109 walitibiwa kwa kutumia mtambo wa Carto 3.
" Matibabu mapya yaliyofanyika katika mtambo wa Cathlab ni upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo wa kurekebisha mishipa ya damu iliyotanuka na kupasuka sehemu ya kifua na tumbo, " Amesema
Na kuongeza " Upasuaji mdogo wa moyo wa kubadilisha valvu ya mshipa mkubwa wa damu (Aortic Valve) bila kufungua kifua (Transcatheter Aortic Valve Implantation procedure — TAVI), kutanua valvu za moyo kwa muda, uchunguzi na kufanya upasuaji wa kuzibua mishipa ya damu ya miguu (Peripheral Interventions) ambayo haipitishi damu vizuri na kuzibua mishipa ya damu ya shingoni, " Amesema.
Katika hatua nyingine na huduma hiyo iwafikie wananchi wengi zaidi wamefungua kliniki mbili za matibabu ya moyo zilizopo Kawe katika jengo la Mkapa Health Plaza na nyingine Oysterbay katika jengo la Oyster Plaza.
" Huduma tunazozitoa ni za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto na watu wazima, kliniki za mishipa ya damu, huduma za maabara (ISO 15189:201), Fiziotherapia (Mazoezi tiba), huduma ya matibabu majumbani, elimu ya afya, lishe bora na mafunzo kwa jamii, huduma ya matibabu ya magonjwa ya ndani, duka la dawa, tiba mtandao, huduma ya gari la wagonjwa na huduma ya upimaji wa afya kwa vikundi mbalimbali, "amesema
Amesema katika kuboresha huduma za afya mtambo wa kuzalisha hewa ya oksijeni uliogharimu shilingi milioni 526,604,116 umefungwa katika Hospitali ya Dar Group pia mtambo mwingine wa kuzalisha hewa ya oksigeni wenye thamani ya shilingi bilioni 1.3 umefungwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
"Mitambo hii inatumika kusambaza hewa ya oksijeni kwa wagonjwa wenye uhitaji na kupunguza gharama za kununua mitungi ya oksijeni kama ilivyokuwa awali na taasisi yetu imesaini mikataba ya miaka mitatu ya makubaliano na Hospitali za Taifa za nchini Rwanda na Zambia ya kutibu wagonjwa wa moyo pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa hospitali hizo wa jinsi ya kuwatibu wagonjwa wa moyo, " Amesema
Pia amesema wamesaini mikataba na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo cha Madaktari wa Upasuaji Afrika Mashariki, Kati na kusini mwa Afrika (COSECSA) katika kutoa mafunzo bobezi ya matibabu ya moyo kwa wataalamu wa afya, Chuo Kikuu cha Jagiellonian cha nchini Poland na Chuo Kikuu cha New York kilichopo nchini Marekani kwa ajili ya kufanya utafiti, elimu na utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa moyo.
Aidha amesema shilingi bilioni 2.16 zilitolewa na Serikali kwaajili ya ukarabati wa vyumba vya watoto mahututi na chumba cha wagonjwa mahututi cha watu wazima, ukarabati na utanuzi wa ICU ya watoto ambayo hapo awali ilikuwa na vitanda nane na hivi sasa inavitanda 16 na ICU ya wakubwa ambayo imetanuliwa na kuwa na vitanda kumi kutoka nane ambapo shilingi 503,450,051 zilitumika katika ukarabati huo. Shilingi 1,465,683,469 zilitumika kununua vifaa tiba, shilingi 170,000,000 zilitumika kwa ajili ya tiba mtandao (Telemedicine) na shilingi 28,340,000 zilitumika kugharamia mafunzo ya wataalamu wa fani ya radiolojia na huduma za wagonjwa mahututi.
Mwisho
0 Comments