Na Costa Sakagoi- Matukio Daima App
WALENGWA Wa TASAF katika wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu wamesema kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini umewaimarisha kiuchumi baada ya kuanzisha miradi midogomidogo ya ujasiliamali inayowaingizia kipato na kuendesha maisha yao.
Nkwaya shigi, mkazi wa Bipyayi ambaye ni mnufaika wa TASAF amesema Mpango huo umebadili maisha yake, kutoka kuwa tegemezi hadi kuwa na kipato chake baada ya kujiunga na Kikundi cha kutengeneza vyungu Bipyayi.
Koga Maduhu, mkazi wa Bipyayi amesema baada na TASAF, kupitia Wanawake wenzake walianzisha kikundi cha Upendo na Gagaja kutengeneza vyungu mradi ambao unawaongezea kipato licha ya kukabiliwa na ukosefu wa soko na usafiri.
Minza Mbesi, mnufaika wa TASAF kutoka Guduwi amesema awali hakuwa na dira ya maisha, lakini baada ya kuingizwa katika Mpango wa kunusuru kaya Maskini amebadili hali ya kipato na kumudu kuhudumia familia baada ya kujiunga kwenye kikundi cha Nyalele.
Minza Ligima, mnufaika wa TASAF kutoka Guduwi amesema kutokana na fedha za TASAF ameweza kuibadili hali ya kiuchumi ikiwemo kujenga nyumba yenye bati 20, kununua kuku, meza na viti lakini pia watoto wake wanatumiza masharti ya kwenye Ruzuku ya Elimu na Afya.
Mratibu wa TASAF wilaya ya Bariadi, Angel Msigwa amesema katika wilaya hiyo walengwa wengi wamejikwamua kiuchumi, wamebadili maisha yao, wanawekeza katika hisa na pia wanashikana mkono kwenye shida na raha.
Ameeleza kuwa walengwa walimeunda vikundi vya kuweka na kukopa na pia wameanzisha miradi midogomidogo ikiwemo kutengeza sabuni, kusindika mbogamboga na ungalishe, kutengeneza vyungu ili kujiongezea kipato.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Bariadi, Khalid Mbwana amesema wanatambua mchango wa TASAF ambao umewatoa kwenye giza mpaka kupata mwanga wa Maendeleo.
"Tuna namba kubwa ya watu wenye hali duni ya maisha, TASAF mmesaidia kubeba huu mzigo na Watu wamehitimu na sasa wanaendesha miradi yao lakini pia tumetekeleza miradi zaidi ya 50 kupitia TASAF" amesema Mbwana.
Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Kitaifa kutoka Mfuko wa Maendeleo TASAF, Richard Shilamba amevipongeza vikundi vilivyonufaika kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Amesema kupitia ziara hiyo wamebaini changamoto ikiwemo ukosefu wa masoko ya bidhaa wanazozalisha na kwamba kupitia maandiko watazingatia mahitaji ya wanufaika na walengwa wa Mpango huo.
0 Comments