Na,Jusline Marco;Arusha
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango amesema Serikali imeendelea kujizatiti kwa kuwekeza katika sekta ya Teknolojia ya habari na mawasiliano ili kuchochea maendeleo na kuwawezesha wananchi kupata huduma za serikali kwa gharama nafuu,Kwa urahisi na mahali popote.
Akifungua Kikao Kazi cha 5 cha Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,Dkt.Mpango amesema uwekezaji kwenye sekta ya tehama umesisitizwa katika kujenga mifumo ya kidijitali katika utendaji wa serikali ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema dira ya maendeleo ya taifa ya 2025 na rasimu ya dira ya taifa ya 2050 zimeitambua Tehama kama nyenzo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ambapo sekta zote za uchumi zitaendeshwa kwa teknolojia ya kisasa.
Ameongeza kuwa serikali ya awamu ya sita itaendelea kuwekeza katika kuwajengea uwezo wataalamu wa Tehama na kada nyingine Kwa kuweka mazingira wezeshi ya ufundishaji kwenye vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu ili viendelee kuzalisha wataalam wa kutosha.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Serikali Mtandao Mhandisi Benedict Ndomba amesema kuanzishwa kwa Mamlaka ya serikali Mtandao kumeiwezesha serikali kuwa na udhibiti wa moja kwa moja wa mifumo ya miundombinu ya Tehama inayotumika serikalini sambamba na kulinda usalama wa taarifa za serikalini.
Mkurugenzi Mkuu wa Serikali Mtandao Mhandisi Benedict Ndomba amesema kuanzishwa kwa Mamlaka ya serikali Mtandao kumeiwezesha serikali kuwa na udhibiti wa moja kwa moja wa mifumo ya miundombinu ya Tehama inayotumika serikalini sambamba na kulinda usalama wa taarifa za serikalini.
Mhandisi Ndomba amesema katika kukabiliana na matishio ya usalama mtandao,Mamlaka hutoa msaada wa kiufundi na ushauri kuhusu usalama wa Tehama na viashitia vya matishio ya kiusalama mtandaoni kwa taasisi za umma pamoja na kukabiliana na mashambulio ya kimtandao pindi yanapotokea.
Amesema katika jitihada za kuendana na mabadiliko ya Teknolojia, mwaka 2019 Mamlaka hiyo ilianzisha kituo cha utafiti ,ubunifu na uendelezaji wa serikali mtandao ambacho hutumika kufanya tafiti na bunifu mbalimbali za mifumo ya Tehama kwa lengo la kutatua changamoto zilizopo nchini na kuboresha utendajikazi serikali na utoaji huduma kwa umma.
Naye Mtendaji Mkuu wa Serikali Mtandao Zanzibar Ndg.Said Said ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mafanikio waliyoyapata katika kusimamia mifumo ya Tehama serikali Mtandao yamerahisisha utoaji wa huduma za serikali kwa wananchi pamoja na kuongeza pato la serikali.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya serikali Mtandao Dkt.Jasmin Tiisekwa amesema dhamira kuu ya serikali ni kuhakikisha serikali inaendeshwa kidijitali na kuwawezesha wananchi kupata huduma za serikali kwa gharama nafuu hivyo Mamlaka iko tayari kupokea, kusimamia na kutekeleza maelekezo yatakayotolewa ili kuweza kuyafikia malengo ya kuijenga serikali ya kidijitali na yenye tija kwa wananchi.
0 Comments