Na Moses Ng'wat, Mbozi.
Mwanaume mmoja ameuawa kwa kuchomwa moto na watu wasiojulikana katika kijiji cha Mbewe, kata ya Mlangali, wilayani Mbozi, baada ya kutuhumiwa kuiba mashine ya kukobolea kahawa na mifuko ya mbolea.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kijijini hapo, ambazo baadaye zilithibitishwa na Jeshi la Polisi, marehemu anadaiwa kuiba vifaa hivyo kutoka kwa mmoja wa wakazi wa kijiji hicho.
"Mwili wa marehemu umekutwa umetetekea vibaya kwa moto asubuhi ya leo, Februari 17, 2025, jambo linaloashiria kuwa huenda alikamatwa na watu hao usiku wa kuamkia leo," kilieleza chanzo chetu.
Inaelezwa kuwa marehemu, ambaye kwa nyakati tofauti alihusishwa na matukio ya uhalifu, ametambuliwa kwa jina la Wizman Mbembela (34), mkazi wa kijiji cha Mbewe, kitongoji cha Iyombo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini wahusika na kuwachukulia hatua za kisheria.
Aidha, Kamanda Senga ametoa wito kwa wananchi kujiepusha na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na badala yake kufuata taratibu za kisheria kwa kutoa taarifa kwa vyombo husika.
Pia amewahimiza kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa zitakazosaidia katika uchunguzi wa tukio hili.
Mwisho.
0 Comments