Header Ads Widget

MAFANIKIO YA TANROADS NA RAIS DKT SAMIA

 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima APP Dodoma

KATIKA kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita kuanzia mwaka 2021 hadi Februari 2025, Serikali imepata mafanikio makubwa katika kuboresha miundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege nchini.

Akiongea na Waandishi wa Habari leo February 17 , 2025 wakati akieleza mafanikio ya miaka 4 ya Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan, Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Ephater Mlavi amesema Katika kipindi hicho barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 15,625.55 zimekuwa katika hatua mabalimbali za utekelezaji ambapo barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 1,365.87 zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami na barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 2,031.11 zimeendelea kujengwa kwa kiwango cha lami. 


Aidha amesema , barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 2,052.94 na madaraja mawili (2) zimefanyiwa Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina na Serikali inatafuta fedha za kuzijenga kwa kiwango cha lami. 


Vilevile, Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina wa barabara zenye jumla ya kilometa 4,734.43 na madaraja kumi (10) unaendelea. 


Aidha amesema , miradi ya barabara yenye urefu wa takriban kilometa 5,326.90 na miradi saba (7) ya madaraja ipo katika hatua ya manunuzi kwa ajili ya kufanyiwa Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina  ikiwa ni maandalizi kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara hizo kwa kiwango cha lami. 

"Katika kipindi tajwa madaraja makubwa 9 yamekamilika kujengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni Shilingi Bilioni 381.301 kama ifuatavyo: Gerezani (Dsm), Daraja jipya la Tanzanite  (Dsm), Wami (Pwani), Kitengule (Kagera), Kiyegeya (Morogoro), Ruaha (Morogoro), Ruhuhu (Ruvuma), Mpwapwa (Dodoma) na daraja la Msingi (Singida), " Amesema. 



Na kuongeza "Madaraja kumi (10) ambayo ni Kigongo  Busisi (Magufuli Bridge - Kilometa 3.0), Lower Mpiji (Meta 140), Mbambe (Meta 81), Simiyu (Meta 150), Pangani (Meta 525), Sukuma (Meta 70), Kerema Maziwani (meta 80), Kibakwe (meta 30), Mirumba (Meta 60) na Jangwani (Meta 390) ujenzi wake unaendelea kwa gharama ya Shilingi Bilioni 985.802," Amesema


Pia amesema Jumla ya Madaraja makubwa kumi na tisa (19) yako kwenye maandalizi ya kujengwa ambayo ni: Godegode (Dodoma), Ugala (Katavi), Kamshango (Kagera), Bujonde (Mbeya), Bulome (Mbeya), Chakwale (Morogoro), Nguyami (Morogoro), Mkundi (Morogoro), Lower Malagarasi (Kigoma), Mtera (Dodoma), Kyabakoba (Kagera), Mjonga (Morogoro), Doma (Morogoro), Sanga (Songwe), Kalebe (Kagera), Ipyana (Mbeya), Mkondoa (Morogoro), Kilambo (Mtwara) na Chemchem (Singida). 


Katika kipindi cha miaka minne (Juni 2021  Des. 2024) hali ya barabara kuu na zile za mikoa imeendelea kuimarika ambapo barabara zilizo katika hali nzuri na wastani zimekuwa karibu asilimia 90 ya jumla ya mtandao wote wa barabara wenye Kilometa 37,225.72 kama inavyoonekana katika Jedwali Na. 2.

 


" Hali hii ya kuimarika kwa mtandao wa barabara imesababisha kupungua kwa muda wa usafiri katika barabara, kuimarika kwa bei za usafirishaji ambapo nauli hazipandi kiholela na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kijamii zinazotumia barabara, " Amesema.


Kwa upande wa viwanja vya ndege, amesema  ujenzi umekamilika kwa miradi Saba (7) ya Julius Nyerere (Terminal Three), Mwanza, Mtwara, Songea, Songwe (Runway), Songwe (Supply and Installation of Airfield Ground Lights (AGL) na Geita. Aidha, ujenzi wa Viwanja vya Ndege Nane (8) ambavyo ni Msalato, Iringa, Musoma, Tabora, Shinyanga, Sumbawanga, Kigoma na Moshi unaendelea.



UDHIBITI WA UZITO WA MAGARI   


Ili kulinda rasilimali za miundombinu ya barabara na madaraja, Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS inafanya udhibiti wa uzito wa magari kulingana na Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Mwaka 2016 na Kanuni zake za Mwaka 2018 ili zisiharibike mapema na ziweze kudumu kulingana na usanifu wake.


Amesema katika kutekeleza jukumu hilo, mizani zinazohamishika na zisizohamishika hutumika. Idadi ya mizani zisizohamishika imeongezeka kutoka 67 hadi 79 na zinazohamishika kutoka 17 hadi 22 kati ya mwaka 2021/22 hadi Julai 2024.


"Katika kupunguza foleni ya magari katika mizani zenye magari mengi, Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS imefunga mizani ishirini (20) za kupima magari yakiwa kwenye mwendo (Weigh-in-Motion WIM) katika Mikoa ya Pwani, Morogoro, Iringa, Songwe, Dodoma, Singida, Arusha na Mara.


 

USHIRIKI WA WAZAWA KATIKA UTEKEZAJI WA MIRADI 


Hali ya Ushiriki wa Makandarasi, Washauri Elekezi na Wanawake katika utekelezaji wa Miradi katika Miradi ya Matengenezo ni ya kuridhisha. Hata hivyo, ushiriki wao katika miradi ya Ujenzi wa Barabara Kuu na Barabara za Mikoa hairidhishi. 


Amesema Idadi ndogo ya wanawake kushiriki kuomba zabuni, Wanawake kusumbuliwa na changamoto za kifamilia zinazowataka muda mwingi kuhudumia familia. 


Hata hivyo Wanawake Wakandarasi wanashauriwa kushiriki kwenye semina zinazoendeshwa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi, kuendelea uhamasishaji na semina mbalimbali za kuwawezesha wanawake kushiriki katika kazi za matengenezo ya barabara


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI