Header Ads Widget

WIZARA YA MADINI KUJA NA KANUNI WEZESHI KWA WACHIMBAJI WADOGO

 

Na Farida Mangube Morogoro 

Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema, kufuatia changamoto zilizobainika katika  uingiaji mikataba ya  utoaji wa misaada ya kiufundi kati ya wamiliki wa leseni ndogo za uchimbaji madini na wawezeshaji, Wizara inaona ni vema kuwepo na Kanuni ambazo zitaweka utarajibu na mazingira wezeshi ya kuingia mikataba hiyo.


Waziri Mavunde amesema hayo leo Februari 17, 2025 wakati akifungua Kikao Kazi cha kupokea maoni kutoka kwa wadau kuhusu mapendekezo ya kuandaa Rasimu ya Kanuni za Madini za Utoaji Msaada wa Kiufundi kwa Wamiliki wa Leseni Ndogo za Uchimbaji Madini za Mwaka 2025 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Edema Hoteli Mkoani Morogoro.



Aidha, Waziri Mavunde ametoa wito kwa washiriki wote wa Kikao Kazi hicho kutoa maoni yao kwa uhuru na uwazi ili kusaidia upatikanaji wa Kanuni nzuri na inayotekelezeka kwa lengo la kuongeza tija katika mnyororo mzima wa shughuli za Sekta ya Madini nchini na kutekeleza sharti la kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Madini Sura Namba 123.


"Katika kipindi cha muda mfupi tumeshuhudia mabadiriko makubwa kwenye Sekta ya Madini kutokana na utashi wa Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anatamani kuona wachimbaji wadogo wanafikiwa, ambapo leo naagiza ofisi ya Kamishna kuwasaidia wachimbaji wadogo ili waweze kugraduate kutoka hapo walipo na kuendelea mbele," amesema Waziri Mavunde.


Pia, Mavunde amewapongeza wachimbaji wadogo kwa kukubari kuuza dhahabu zao Benki Kuu ya Tanzania ambapo ndani ya miezi minne Benki Kuu imenunua zaidi ya tani 2.4.



"Serikali imetenga maeneo yenye taarifa za Utafiti kwa wachimbaji wadogo ambapo mpaka sasa nchi yetu imefanyiwa Utafiti wa low resolution geological survey kwa asilimia 100, Utafiti wa Jiofizikia kwa asilimia 97, Jiokemia kwa asilimia 24 na Utafiti wa kina wa High resolution Geophysical Surgery kwa asilimia 16 pekee, hivyo kukiongeza wigo wa Utafiti naamini Wachimbaji Wadogo wataongeza uzalishaji na mchango zaidi ya ilivyo sasa," amesema Waziri Mavunde.


Pamoja na mambo mengine, Waziri Mavunde ametoa onyo kwa wachimbaji wadogo kutowakaribisha wageni bila kufuata utaratibu katika leseni za uchimbaji mdogo wa madini ambapo itapelekea kufutiwa leseni kwa atakaye kiuka agizo hilo na kutoa angalizo kwa Maafisa Madini Nchini kudhibiti uingiaji wa wageni bila kufuata taratibu.


Pia, amelitaka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuendelea kulea wachimbaji wadogo kwa vitendo ili kusaidia upatikanaji wa ajira na kuongeza tija kwenye mnyororo mzima wa shughuli za uchimbaji na uzalishaji wa madini nchini.


Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo  amesema Kikao hicho kimelenga kupokea mapendekezo ya wadau kwa ajili ya kuandaa rasimu ya Kanuni za Msaada wa Kiufundi kwa ajili ya wamiliki wa leseni za uchimbaji mdogo ambapo Wizara iko huru na tayari kupokea maoni ya kila mdau.


Naye, Rais wa Wachimbaji Wadogo wa Madini Nchini Tanzania John Bina amempongeza Waziri Mavunde kwa uamuzi wa kuwashirikisha wadau wa Sekta ya Madini wakiwemo wachimbaji wadogo ili kuandaa rasimu ya Kanuni hizo kuliko kujifungia na kuandaa Wizara pekee.


Kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa Wachimbaji Wadogo kutoka mikoa yote nchini, vyama vya wachimbaji wadogo wanawake Tanzania na wafanyabiashara wa madini nchini.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI