Header Ads Widget

MADIWANI KIGOMA UJIJI WACHARUKA WATAKA WAKANDARASI WANAOKWAMISHA MIRADI WAONDOLEWE



Na Fadhili Abdallah,Kigoma


MADIWANI katika halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji wakiongozwa na Meya wa manispaa hiyo Baraka Lupoli wamezikataa kampuni za ukandarasi zinazotekeleza miradi ya masoko na miradi ya miundo mbinu inayotekelezwa kwa fedha za mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia (WB).


Kauli hiyo ya madiwani inafuatia ziara waliyofanya kupitia kamati ya kudumu ya fedha na uongozi ya baraza la madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kutembelea miradi hiyo inayotekelezwa kupitia Mradi wa kuendeleza na kuboresha  Miji  Nchini Tanzania ( TACTICS) ikiwa na thamani ya shilingi Bilioni 46.2.



 Mradi wa ujenzi wa soko la Mkakati la Mwanga na Soko la uchakataji wa mazao ya uvuvi Katonga mradi wenye thamani ya shilingi Bilioni 16.4  Diwani wa kata ya Bangwe, Hamisi Berese  alionyesha kutoridhishwa na kazi inayofanywa hadi sasa na wakandarasi wa mradi huo wakandarasi wazawa M/S Asabhi Co. Ltd. na Pioneer Builders Ltd  akitaka wakandarasi hao watimuliwe.



Kwa upande wake Diwani wa kata ya Mwanga Kaskazini ambapo mradi huo unatekelezwa, Sharon Mashanya akizungumza huku akilia alikusudia kuvua nguo ili amwage radhi kuonyesha hasira yake kwa wakandarasi kushindwa kutimiza majukumu yao na kumuomba Raisi Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua kwa wale wote wanaokwamisha utekelezaji wa mradi huo.


Sambamba na mradi huo Madiwani hao pia walitembelea mradi wa ujenzi wa barabara ya lami kilometa 9.4 mradi ulioanza November mwaka 2023 wenye thamani ya shilingi Bilioni 29.8 kwa kipindi cha Miezi 15 ukitekelezwa na Kampuni ya China CRJE   EAST AFRICA ambapo utahusisha Ujenzi wa Barabara ya Wafipa hadi Kagera yenye urefu wa Km 2.434, Daraja la Mto Ruiche, Ujenzi wa barabara ya Bangwe hadi Burega- Ujiji yenye urefu wa Km 7.1, na Ujenzi wa mitaro ya kutiririsha maji ya Mvua katika maeneo ya Bangwe,  Burega,  Rutale,  Mlole , Bushabani, Mji mwema,  na Katonyanga yenye urefu Km 5.288.


Mradi huo ulipaswa kukaamilika Februari 20 mwaka huu lakini hadi sasa  haujafika hata asilimia 50 ya utekelezaji ambapo Diwani wa kata ya Rubuga, Omari Gindi alisema kuwa wakandarasi hao wanafanya masihara na utekelezaji wa miradi hiyo na kuitaka Wizara ya Tawala za mikoa na serikali za  mitaa kuchukua hatua kwa kuwaondoa wakandarasi hao kwani wameonyesha wazi hawana dhamira ya kweli ya kutekeleza miradi hiyo.


Akihitimisha kuhusu miradi hiyo Meya wa manispaa ya Kigoma Ujiji, Baraka Lupoli alisema kuwa Halmashauri imeshatoa tamko la kutokuwa na nia ya kuendelea na wakandarasi hao lakini pia ameitaka TAMISEMI kuchunguza kamati zinazopitia maombi na kuwapitisha wakandarasi kwani kwenye miradi hiyo ya Kigoma kuna walakini mahali katika kuwachagua wakandarasi ikiwemo tuhuma ya rushwa.



Akizungumza katika ziara hiyo Mwakilishi wa kampuni ya Saba Engineering,  John Meena ambaye amemwakilisha Mhandisi  Mshauri wa miradi hiyo alisema kuwa wametekeleza majukumu yao ikiwemo kuwasilisha taarifa zote za maendeleo ya mradi TAMISEMI na mapendekezo yah atua za kuwachukulia wakandarasi hao.


Meena alisema kuwa Pamoja na hayo zipo changamoto zinazofanya kuchelewa kwa mradi ambapo Wakandarsi wametaka kupewa msamaha wa kodi kwa ajili ya kununua vifaa vya ujenzi lakini utekelezaji wa maombo hayo umekuwa ukichukua muda mrefu sambamba na uwepo wa mvua na masuala ya fidia kwa wananchi kwenye baadhi ya maeneo wanayopitisha mradi ambapo wananchi wanataka fidia wakati mradi hauna kipengele cha kulipa fidia.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI