Header Ads Widget

UELEWA MDOGO WA MADHARA YA KUTOKUMALIZA DOZI KUNAVYO HATARISHA AFYA YA WANANCHI.

Na Zacharia Nyamoga 

UELEWA mdogo juu ya Athari za kutokumaliza Dozi miongoni mwa wagonjwa kuna hatarisha Afya za wananchi wengi nchini Tanzania hasa waliopo maeneo ya vijijini ambako upatikanaji wa huduma ya Afya si wakuridhisha kitendo kinacho chochea usugu  Dawa.

Kwa mujibu wa Sera ya Afya ya Tanzania ya 2007 kifungu cha 5.1 kinasisitiza umuhimu wa jamii kuwa na Elimu kuhusu matumizi sahihi ya Dawa pamoja na kufahamu madhara yatakayojitokeza endapo mgonjwa hatafuata ushauri wa wataalamu, ikiwa ni moja ya hatua ya kuimarisha Afya ya wananchi kuanzia ngazi ya Kaya hadi Taifa.

Mbali na Sera kueleza bayana kusudi la kuimarisha Afya ya wananchi bado hali inaonekana kuwa tofauti kwa baadhi ya Wananchi kutoka Kata ya Kimala Wilaya Kilolo kwenye Zahanati mbili pekee zinazohudumia Vijiji zaidi ya vitano (Ndege Sivili, Idunda, Mhanga, Itonya, Uluti, na Kimala yenyewe) ambako baadhi ya wagonjwa huacha Dozi njiani punde wanapohisi nafuu na kuzihifadhi kwa matumizi ya siku wanapohisi dalili za ugonjwa.

Moja ya wananchi aliyejitambulisha kwa jina la Adelina Kigae ameiambia Matukio Daima analazimika kutunza Dawa katika kifungashio chake kwa ajili ya matumizi ya siku atakapo hisi dalili za homa au ugonjwa wa gafla hasa nyakazi za usiku kutokana na ukosefu wa Zahanati kijijini hapo.

"Kama unavyoiona miguu yangu ilivyo vimba na huu uzee kutoka hapa kijijini Idunda hadi kituo cha Afya cha Kidabaga ni mbali kwenda na kurudi natumia siku nzima au hata zaidi sasa haya maisha yalivyo nalazimika kutunza tu dawa katika mfuko nikiugua nameza" Alisema Bi. Kigae Mkazi wa Kijiji cha Idunda 

Hoja ya Bi. Kigae inaungwa Mkono na Mzee Luka Kalinga mkazi wa Kijiji cha Mhanga kilichopo kata ya Kimala ambaye kwa muda mrefu amekuwa akitunza dawa mbalimbali katika kifungashio ambacho amekihifadhi juu ya paa la nyumba yake "hizi dawa ninazo za toka mwaka 2020 nikipata homa Mimi, mke wangu au mtoto hapa tunameza " Alisema Mzee Luka huku akinionesha lundo la Dawa mchanganyiko zilizo katika mfuko wa lailoni zikiwa na maandishi ya kitabibu.

Bi Kigae na Mzee Luka ni baadhi tu ya wananchi wachache kati ya wengi wanao akisi maisha halisi ya wananchi walio maeneo ya vijijini hasa kwa maeneo ambayo hayana kabisa Zahanati kama Kijiji cha Idunda, Mhanga na Uluti katika Kata hii ya Kimala.

Kufahamu usalama wa wananchi hawa upo kwa kiwango gani Matukio Daima tumefanya mahojiano na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo Dkt. Clemence Konkamkula ambaye alitoa uwito kwa wananchi kufuata ushauri wa wataalamu wa Afya kabla ya kutumia dawa na wafuate maelezo yote yanayotolewa na wahudumu wa Afya.

“Wapo baadhi ya wagonjwa ambao huacha kutumia dozi punde wanapojihisi nafuu na kuzitunza kwa matumizi ya siku anapohisi tena ugonjwa jambo hili ni hatari sana kwa Afya, kutomaliza dawa kunaweza kusababisha usugu wa dawa (drug resistance), ambapo vimelea vinajifunza kupinga dawa, na matibabu yanakuwa magumu zaidi, hii inaweza kusababisha magonjwa sugu kama vile 'multi-drug resistance' au 'extensively drug resistance,' hali inayoongeza changamoto kwa mgonjwa na mfumo wa afya,” alisema Dkt. Clemence

Aidha ameongeza kuwa tatizo la kutomaliza Dozi miongoni mwa wagonjwa linaonekana ni kubwa zaidi hasa kwa wagonjwa wanaotumia dawa za muda mrefu kama vile Tuberculosis (TB) na wagonjwa wanaoishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

"Baadhi ya wagonjwa wanaotumia dawa za muda mrefu hasa kuanzia Miezi sita au zaidi wengi wanakimbia dawa na hawafiki katika vituo walivyo jiandikisha kwa ajili ya kuchukua dawa hii inatupa wakati mgumu sana wataalamu wa Afya kwani tunaenda kutengeneza bomu kubwa na hatari kwa Afya" Alisisitiza Dkt. Clemence

Mohamed Mwenga ni mdau wa Afya kutoka shirika la USAID Afya yangu Kanda ya kusini ameshauri wadau na serikali kuchukua hatua za haraka kutoa elimu kwa wananchi kwani wengi wao wamekuwa wakisitisha dawa kutokana na hali duni ya maisha na kutokuwa na uelewa wa kina kufahamu madhara yake.

"Wananchi wengi hasa walio maeneo ya vijijini wanaishi kwa mazoea akihisi homa haendi kupata vipimo ajue shida ni nini yeye anameza dawa yeyote kati ya zile alizo zihifadhi sasa hii ni hatari sana na hapa serikali kwa ushirikiano na wadau mbalimbali kuvaa jukumu la kutoa Elimu Kaya kwa Kaya, Kijiji kwa Kijiji" Alisema Dkt. Mwenga

Tatizo la kutomaliza Dozi na kutumia dawa bila kufuata ushauri wa wataalamu wa Afya lina athari si tu kwa Afya ya mgonjwa mmoja mmoja bali hata kwa mfumo wa Afya hivyo Elimu kwa jamii na kuboresha miundombinu ya Afya na kupunguza gharama za dawa ni hatua muhimu za kupunguza ukubwa wa athari za tatizo kama ilivyobainishwa na Dkt. Mwenga ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha ushauri wa wataalamu wa Afya unafuatwa ili kujenga jamii yenye Afya Bora na Salama



 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI