Na,Jusline Marco;Arusha
Tanzania imepata fursa ya kuwa wenyeji wa Mkutano wa 73 wa Baraza la Kimataifa la Viwanja vya Ndege kwa Kanda ya Afrika ambao utaambatana na Maonesho ya Wadau utakaofanyika Aprili 24 hadi 30, 2025 jijini Arusha na kutanguliwa na mkutano mkuu,mikutano ya bodi na mikutano ya kamati mbalimbali za kitaalam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Waziri wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa amesema tukio la Nchi kuwa wenyeji wa mkutano huo ni muendelezo wa Mafanikio ya kimkakati yanayoendelea kupatikana kupitia viwanja vya ndege.
Prof.Mbarawa amesema mkutano huo utakuwa na faida mbalimbali kwa nchi ikiwemo kuwaongezea ujuzi wazawa katika masuala ya usafiri wa anga na utaliu kupitia kujifunza mbinu bora za kimataifa zinazitumika katika kuboresha sekta hizo,kutoa fursa kwa wazawa kujifunza kuhusu utoaji wa huduma bora na ufanisi wa utendaji kazi katika sekta hizo.
Ameongeza kuwa lengo la mkutano huo ni kukutanisha nchi wanachama ili kujadili juu ya changamoto zinazokabili viwanja vya ndege lengo likiwa ni kuhakikisha kunakuwepo na uendelevu,usalama na ufanisi katika usafiri wa anga sambamba na uzingatiaji wa masuala ya kimazingira katika viwanja vya ndege.
Pamoja na hayo Prof.Mbarawa amesema sekta ya Anga inakabiliwa na Shinikizo la kupunguza utoaji wa hewa ukaa hivyo kupitia mkutano huo wanachama watapata zana,maarifa na mikakati stahiki ya kupunguza hewa ukaa kupitia utekelezaji teknolojia kijani ambayo itachangia katika ukiaji endelevu wa kiuchumi.
Ameeleza kuwa serikali ya awamu ya sita itaendelea kuweka mazingira rafiki ya kuifanya nchi kuwa sehemu ya utalii wa mikutano mikubwa ya kimataifa Barani Afrika.
Mkutano huo utaenda sambamba na kaulimbiu ya "Katika kuelekea wakati ujao Bora wa Kijani;kutumia usafiri wa Anga endelevu na Utalii kwa Ustawi wa Kiuchumi."ambapo Mkutano huo utaleta pamoja wajumbe 400 kutoka nchi 54 za Bara la Afrika ambazo ni wanachama wa Baraza hilo la Kimataifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya viwanja bya ndege TAA Bwn.Abdul Mombokaleo amesema kuwa Mamlaka ya viwanja vya ndege inatambua jitihada za Wizara za kuhakikisha TAA inaimarika kiitendaji kwa kuhakikisha inaongezewa Ruzuku katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Amesema katika kuhakikisha TAA inaendana na kasi ya mabadiliko yanayofanywa na serikali ya awamu ya sita,menejimenti imejipanga kuviwekea vipaumbele vya msingi kuhakikisha inaboresha utendaji wa kazi na huduma katika viwanja vya ndege kwa kuimarisha matumizi ya mifumo ya tehama kwenye shughuli za uendeshaji na biashara katika viwanja vyote vya ndege.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo amesema viwanja vya ni sekta mtambuka kutokana na uwepo wa wadau wengi walio ndani ya viwanja vya ndege wanaoshiriki kibiashara ambapo amesema kufanyika kwa mkutano huo jijini Arusha ni fursa kwa nchi kuweza kujitangaza.
0 Comments