Na Moses Ng'wat, Tunduma.
WATAALAM wa sekta ya afya Mkoani Songwe wamejipanga kutekeleza mikakati madhubuti yenye lengo la kuhakikisha uendelevu wa usimamizi na utoaji wa huduma bora za afya.
Mikakati hiyo imebainishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Boniface Kasululu, wakati akiongoza kikao maalum cha uhakiki na tathmini ya ubora wa takwimu za huduma za afya, kilichofanyika Januari 16, 2025 katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Tunduma.
Dkt. Kasululu amesisitiza umuhimu wa takwimu katika mfumo wa utoaji huduma za afya nchini.
"Takwimu ni moja ya nguzo kuu za mfumo wa utoaji huduma za afya katika nchi, lakini pia ubora wa takwimu ni msingi wa maamuzi sahihi na ya ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi," alisema Dkt. Kasululu.
Aidha, Dkt. Kasululu amesisitiza umuhimu wa utoaji wa huduma bora kwa wananchi, akibainisha kuwa serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya maboresho makubwa katika sekta ya afya.
Ameeleza kuwa maboresho hayo ni pamoja na kuleta vifaa tiba, ujenzi wa hospitali, na vituo vya afya pamoja na kuajiri watumishi.
"Miaka mitano iliyopita, Mkoa wa Songwe ulikuwa hauna hospitali ya mkoa, na ni Halmashauri tatu pekee ndizo zilikuwa na hospitali, lakini sasa hata Halmaahauri yenu ina Hoapitali kubwa " alisema Dkt.Kasululu.
Hata hivyo, alibainisha kuwa changamoto kubwa iliyosalia ni kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa.
"Deni kubwa tulilonalo ni kuhakikisha ubora wa huduma tunazotoa unakuwa wa kiwango cha juu na sisi kama watoa huduma, ni jukumu letu kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora," alisisitiza.
Dkt. Kasululu alisema kwa mwaka huu, Mkoa wa Songwe umejipanga kuhakikisha usimamizi wa huduma za afya unaimarishwa zaidi kupitia mshikamano wa viongozi na watumishi wa afya.
Aliwataka waganga wakuu wa wilaya, halmashauri, na menejimenti za hospitali kushirikiana kufanikisha maboresho hayo.
Katika kikao hicho, timu ya wataalam kutoka ngazi ya Mkoa wakiongozwa na Dkt. Kasululu itafanya tathmini ya takwimu za huduma za afya za kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2024.
Timu hiyo pia imepanga kutembelea vituo vya afya nane ndani ya siku mbili zijazo na kuandaa mpango kazi wa kuboresha vituo vingine vilivyobaki kabla ya mwisho wa Februari 2025.
"Kazi hii ta maboresho haina gharama yeyote na bahati nzuri vituo vyenu vipo ndani ya umbali unaofikika, hivyo tunapaswa kumaliza zoezi hili kwa wakati," alibainisha Dkt. Kasululu.
Alisisitiza kuwa, baada ya kikao kazi hicho, maboresho kama hayo yatafanyika katika Halmashauri nyingine zote za Mkoa wa Songwe.
0 Comments