Na Fadhili Abdallah,Kigoma
RAISI Samia Suluhu Hassan amekabidhi misaada mbalimbali ya vyakula na mahitaji ya kibinadamu kwa wazee wasiojiweza wanaolelewa katika kituo cha kulea wazee Kigoma ikiwa ni mchango wake katika kujali maisha ya wazee hao.
Misaada hiyo yenye thamani ya shilingi milioni 2.1 ilikabidhiwa kwa uongozi wa kituo hicho na Mkuu wa wilaya Kigoma,Dk.Rashid Chuachua akimwakilisha Mkuu wa mkoa Kigoma, Thobias Andengenye ambaye alipaswa kukabidhi misaada hiyo kwa niaba ya Raisi Samia.
Akikabidhi misaada hiyo Mkuu huyo wa wilaya Kigoma alisema kuwa Rais Samia ametoa misaada hiyo akithamini mchango wa wazee kama kundi muhimu kwa jamii hivyo amewiwa kutoa misaada hiyo ili kuona wazee hao wanaishi na kufurahia maisha yao kama binadamu wengine.
Akizungumzia kutolewa kwa misaada hiyo Katibu wa kambi hiyo ya Wazee Veronica Ramadhani amemshukuru Rais Samia kwa msaada huo na kumuomba Mwenyezi Mungu azidi kumbariki na kuwapatia misaada zaidi.
Sambamba na hilo Katibu huyo amelalamikia wizi unaotokea kituoni hapo hasa misaada inayotolewa na mazao yanayolimwa hivyo wameomba serikali kuangalia namna ya kuwajengea uzio ili kuondokan na kadhia hiyo.
0 Comments