Mwandishi wa Matukio Daima media Francis Godwin akimpongeza mbunge wa Viti maalum mkoa wa Iringa Ritta Kabati baada ya Kumaliza mahojiano kupitia kipindi Cha Tanzania ya Leo kinachorushwa na Matukio Daima Tv
Na Matukio Daima media
Katika jitihada za kuboresha maisha ya mtoto wa kike na kuhakikisha kwamba wanapata nafasi ya kuendeleza maisha yao kwa njia bora, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa, Ritta Kabati, ameandika historia muhimu.
Kupitia juhudi zake za zaidi ya miaka 10 katika siasa, Kabati ameweza kubadilisha maisha ya mabinti wengi ambao awali walikimbilia mijini kufanya kazi za uyaya na wengi kuwaita Ma TX .
Akizungumza na kipindi Cha Tanzania ya Leo kinachorushwa na Matukio Daima Tv jana Kabati anasema alijitosa katika harakati hizi kabla ya kuingia rasmi kwenye siasa, akianzisha mpango wa kutoa elimu kwa watoto wa kike.
Kwani aliona umuhimu wa kuzuia mwelekeo wa mabinti kwenda mijini kufanya kazi za ndani, hali ambayo mara nyingi hupelekea changamoto za kiuchumi, kijamii, na hata kimaadili.
Hivyo kupitia mpango huu wa elimu, alihamasisha jamii kuelewa thamani ya kusomesha watoto wa kike badala ya kuwaona kama njia ya kipato kwa familia kupitia ajira za ndani.
Mbunge huyo alisema kuwa elimu ni nyenzo muhimu ya kumkomboa mtoto wa kike kutoka kwenye mzunguko wa umaskini.
Kuwa mabinti waliopata elimu walikuwa na nafasi nzuri ya kuboresha maisha yao na ya familia zao, tofauti na wale waliokwenda mijini kufanya kazi za ndani ambazo mara nyingi ni za kipato kidogo na mazingira magumu.
"Baada ya kuona mafanikio ya mpango wake wa elimu, Kabati alianzisha SACCOs ya kusaidia mabinti na wanawake kiuchumi"
Alisema kuwa kupitia SACCOs hii, inayojulikana kama Wekeza Uwezeshwe, zaidi ya vijana 400 walihusishwa katika mpango wa kuboresha maisha yao.
Kabati alisema Mabinti waliokimbilia mijini walirudishwa vijijini na kusaidiwa kupata ajira zenye staha au kuanzisha miradi ya kiuchumi
SACCOs hiyo ilikuwa daraja muhimu kwa wanawake na mabinti wa Iringa, kwani iliwapatia mikopo ya mitaji kwa ajili ya kuanzisha biashara ndogo ndogo.
" Hili liliwawezesha kujitegemea kiuchumi, huku wakibaki karibu na familia zao badala ya kuhama na kwenda mijini kufanya kazi za ndani"
Pamoja na mafanikio haya, Kabati anakiri kuwa alikumbana na changamoto kubwa kutoka kwa baadhi ya watu waliokuwa wakimuona kama kikwazo kwa familia zilizotegemea kipato kutoka kwa mabinti waliokwenda mijini.
" Watu walimchukia kwa sababu ya msimamo wake wa kukemea vikali tabia ya kuwaruhusu mabinti kwenda mijini kufanya kazi za ndani"
Hata hivyo alisema alisimama imara na kuendelea kuelimisha jamii kuhusu athari za kuwaacha mabinti wao kwenda mijini bila uangalizi.
Alisema kupitia Ritta Kabati Trust, aliweza kutoa msaada zaidi kwa wanawake na mabinti, huku akiendelea kuboresha mazingira ya kielimu na kiuchumi kwa watoto wa kike wa mkoa wa Iringa.
Juhudi za Kabati zimezaa matunda, kwani sasa kuna ongezeko kubwa la mabinti wanaobaki vijijini kwa ajili ya masomo badala ya kukimbilia mijini kufanya kazi za uyaya.
Kwani kupitia taasisi yake, ameendelea kuwahamasisha wanawake kuwalea mabinti wao kwa kuwapa elimu bora na kuwajengea msingi wa maisha ya kujitegemea.
Kabati alisema kuwa tasisi ya Ritta Kabati Trust pia imejikita katika kuwasaidia vijana na wanawake kupata mafunzo ya ujasiriamali. Mafunzo haya yamewapa stadi muhimu za maisha, na hivyo kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi zinazoboresha maisha yao na ya familia zao.
Aidha Kabati amepongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya makundi maalum ya vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu.
Kuwa mikopo inayotolewa kupitia halmashauri kwa makundi haya imekuwa msaada mkubwa katika kuboresha maisha ya wengi.
Kwa mujibu wa Kabati, mkakati wa serikali wa kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake umekuwa chachu kubwa ya maendeleo.
Kuwa ni pamoja na kusaidia wanawake wanaolea watoto wenye ulemavu ambao mara nyingi hukumbana na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na kutelekezwa na wenzi wao.
Hata hivyo alisema Kupitia mikopo hiyo, wanawake hao wameweza kuanzisha miradi ya kiuchumi inayowawezesha kuwalea watoto wao katika mazingira bora.
Pia Mbunge Ritta Kabati ameeleza kuwa moja ya malengo yake makubwa ni kuhakikisha kwamba wanawake wanaoishi na watoto wenye ulemavu wanapata nafasi sawa za kiuchumi.
Kuwa ameweka mkakati wa kuhakikisha kwamba sehemu ya mikopo inayotengwa na halmashauri inaelekezwa kwa wanawake hawa.
Alisema kuwa changamoto kubwa wanayokutana nayo wanawake wanaolea watoto wenye ulemavu ni ukosefu wa mitaji na msaada wa kifamilia, kwani mara nyingi hukimbiwa na wenzi wao.
Kuwa kupitia pesa zinazotengwa kwa makundi maalum, wanawake hawa wataweza kupata mitaji ya kuanzisha biashara ndogo ndogo na hivyo kujitegemea kiuchumi.
Mbunge Kabati ameonesha mfano wa kiongozi anayejali ustawi wa jamii, hasa kwa watoto wa kike na wanawake.
Hivyo jitihada zake zimekuwa msaada mkubwa kwa mkoa wa Iringa, na mafanikio yake yanaendelea kuhamasisha viongozi wengine kuwekeza katika elimu na maendeleo ya kiuchumi kwa wanawake na vijana.
Ikumbukwe kuwa kupitia taasisi yake na ushirikiano na serikali, Kabati ameweza kuleta mabadiliko makubwa, huku akiwapa mabinti na wanawake wa Iringa fursa ya kuboresha maisha yao na ya familia zao.
Hii ni Historia yake na ni mfano wa kujivunia na inaonyesha jinsi kiongozi mmoja anavyoweza kuwa na athari kubwa kwa jamii.
TAZAMA MAHOJIANO KUPITIA CHANEL YA MATUKIO DAIMA TV
0 Comments