Na Thobias Mwanakatwe,Itigi
WAJASIRIAMALI 6,500 katika kata 13 zilizopo Halmashauri ya Itigi wilayani Manyoni mkoani Singida wameanza kupatiwa mafunzo yatakayowawezesha kujikwamua na umaskini na pia kukidhi vigezo vya kupata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa wanawake,vijana na watu wenye ulemavu.
Mtendaji wa Kata ya Itigi mjini, Saimon Sirilo, ambaye anaendesha mafunzo hayo kwa kujitolea alisema hayo juzi wakati akitoa mafunzo kwa wananchi 166 wa kata ya Mitundu.
Alisema ameamua akiendesha mafunzo hayo tangu Januari 2024 kwa wananchi ili waweze kuwa na mbinu za kuanzisha biashara ndogondogo zitakazowakwamua kiuchumi pamoja na kuunda vikundi ambavyo vitawafanya wapate mikopo inayotolewa na halmashauri.
Alisema mafunzo anayoyatoa kwa wananchi wanaopenda kujiingiza kwenye ujasiriamali ni jinsi ya kutengeneza sabuni ya maji, batiki,karanga za mayai, elimu ya fedha,jinsi ya kupanga bajeti,huduma kwa wateja na namna ya kutafuta masoko
Sirilo alisema hadi kufikia Disemba 2024 ametoa mafunzo hayo kwa wajasiriamali wa kata 10 za Halmashauri ya Itigi ambazo ni Majengo, Itigi mjini,Tambukareli, Ipande, Sanjaranda,Aghondi,Mgandu,Mitundu,Mwamagembe na Kitaraka.
Alisema kata zilizobaki ambazo ni Kalangali,Rungwa na Idodyandole anatarajia ndani ya mwezi huu (Januari) atamalizia kufanya mafunzo na kwamba tangu ameanza kufanya kazi hiyo kumekuwa na mwitikio mzuri kutoka kwa wananchi.
"Mafunzo hayo nayatoa bure katika maeneo yote kama sehemu ya utumishi wangu kwa kuwahudumia wananchi nikiamini kuwa jamii ikikombolewa kimaarifa na kiuchumi basi taifa limepona na tutakuwa na maendeleo makubwa katika taifa letu," alisema.
Sirilo aliwashukru viongozi wa kata hususani madiwani ambao katika kila kata anayokwenda kutoa mafunzo amekuwa akipata ushirikiano mzuri na hivyo mafunzo kufanyika kwa ufanisi mkubwa.
Mwishoni mwa mwaka jana Halmashauri ya Itigi ilitoa wito kwa vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu kuchangamkia kuomba mikopo ambapo zaidi ya Sh.milioni 442.755 zimetengwa kwa ajili ya kutoa mikopo hiyo kwa vikundi hivyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Itigi,Ayoub Nkambi, alisema fedha hizo zilianza kutengwa katika robo ya kwanza ya Julai-Septemba ya mwaka wa fedha 2024/2025.
"Halmashauri ya Wilya ya Itigi inatangaza uwepo wa fedha kwa ajili ya kuvikopesha vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ambapo jumla ya Sh. 442,755,221.17 zimetengwa, vikundi vyenye sifa vinakaribishwa kuleta maombi katika Ofisi za serikali za Vijiji zilizopo katika maeneo yao," alisema.
Nkambi amesema vikundi vinavyotakiwa kuomba mikopo ni kile ambacho kinatambuliwa na kupewa cheti cha utambuzi na halmashauri, kinachojishughulisha na shughuli za ujasiriamali mdogo au wa kati au kikundi kinachotarajia kuanzisha shughuli za ujasiriamali.
Amesema sifa nyingine kwa kikundi cha wanawake na vijana lazima kiwe na idadi ya wanakikundi kuanzia watano na kuendelea na kikundi cha watu wenye ulemavu kiwe na wanakikundi wasiopungua wawili .








0 Comments