Header Ads Widget

MEYA SINGIDA ATAKA VIJIWE VYA KUCHEZA MCHEZO WA BAO VITUMIKE KUTOA USHAURI WA MAENDELEO

 

Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA

MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Singida, Yaghi Kiaratu, amevitaka vijiwe ambavyo vinatumika kwa ajili ya kucheza mchezo wa bao kwa wazee kutoa ushauri utakaowezesha Singida kupiga hatua kimaendeleo.

Ametoa ushauri huo juzi wakati akizungumza na wanachama wa kikundi cha Amani aambacho kiliandaa hafla fupi ya kuwapa zawadi washindi watatu waliopatikana baada ya kufanyika ligi ya manispaa.


“Mchezo huu wa bao waasisi wetu wa taifa wakati wanatafuta uhuru waliutumia kwa ajili ya kuzungumzia siri za uhuru hivyo na sisi tutumie bao hili kuijenga singida yetu kwa maendelei sio kwa majungu,” alisema.

Kiaratu alisema mchezo huo ambao unapendwa zaidi ya wazee ushauri wao watakaoutoa kwa vijana na kuangalia maadili ya watoto Sigida itaendelea kuwa ya amani.

Alisema kikundi cha Amani kikisajiliwa na kutambulika kinaweza kama fursa ya kupata mikopo kwenye taasisi za fedha na kuahidi kutoa gharama zote ili kiweze kusajiliwa.

“SISI mjini hatuna mashamba, mashamba yetu ni kujishughulisha na kazi mbalimbali, huyu atauza mtumba, yule atauza kuku ndio mashamba yetu, kikundi hiki badala kucheza bao mtaenda kwenye mchezo wa kuwekeza na mkawa mnapeana mitaji hivyo mkainuana kiuchumi,” alisema.

Alisema kujishughulisha na kazi za kufanya kunaepusha kujiingiza katika mambo mabaya ambayo si tu kwamba yanafanywa na vijana lakini pia wazee wanaweza kuyafanya.

“Kundi lenu hili ni muunganiko wa watu wengi ambao wametoka maeneo mbalimbali katika Manispaa ya Singida,kwa hiyo ni lazima kitambulike kwa kukisajili na mimi naahidi nitalipia gharama zote za usajili ili ikitokea fursa mnapata mikopo kupitia kikundi,” alisema.

Naye Mratibu wa Kikundi cha Amani, Dk.Philip Kitundu,alisema ligi ya mchezo wa Bao ilianza Disemba 1, 2024 na kuhitimishwa Disemba 20 mwaka jana ambapo washindi watatu walipatikana ambao ni Dragon, Adam na Omari ambao ndio waliopewa zawadi mbalimbali ikiwamo kuku jogoo.

"Ligi ilishirikisha watu 15 yaani timu 15 na kila timu ilicheza mechi mbili na timu pinzani  na kila timu iliyopata ushindi kwa mechi moja ilipewa pointi tatu," alisema Dk.Kitundu.

Aidha,Dk.Kitundu alimuomba Meya kukisaidia kikundi ili kiweze kupata mkopo halmashauri na kusaidia kiweze kusajiliwa ombi ambalo alilikubali kusaidia fedha za kukisajili.

"Kikundi cha Amani kina wajasiriamali,wafanyabiashra ndogo ndogo na kwa kutumia biashara zetu tukipata mkopo tutaweza kujiongezea kipato na tupo tayari kurejesha fedha hizo kwa wakati kwa kuzingatia masharti ya mkopo,"alisema Dk.Kitundu.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI