Header Ads Widget

KUNDO ATAKA JAMII KUTUNZA VYANZO VYA MAJI.

 


Na Moses Ng'wat,Mbozi.

NAIBU Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew ametoa maelekezo kwa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Rukwa kuhakikisha wanatunza na kuhifadhi rasilimali za maji na vyanzo vyake, ikiwemo kutoa elimu kwa jamii ili huduma za maji ziwe endelevu.

Ametoa maelekezo hayo leo, Januari 13, 2025, mara baada ya kuzindua miradi ya maji katika vijiji vya Ileya na Sambewe, wilayani Mbozi, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya siku mbili mkoani Songwe.

Akizungumza na viongozi na wananchi wa vijiji hivyo, Mhandisi Kundo alisema changamoto za maji katika vijiji vya Ileya na Sambewe katika  kata ya Itumpi ni kubwa na sasa zimepatiwa ufumbuzi baada ya kukamilika kwa miradi hiyo iliyogharimu shilingi milioni 120.



Miradi hiyo, iliyoanza utekelezaji wake tangu Oktoba 11 2024, imetekelezwa kwa juhudi za Mbunge wa Jimbo la Mbozi, George Mwenisongole, kwa kushirikiana na washirika wake.


Miradi hiyo ya maji imehusisha, Uchimbaji wa visima viwili vyenye uwezo wa kuzalisha lita 4,800 na 6,200 kwa saa, ujenzi wa matenki mawili kwa ajili ya usambazaji.


Pamoja na vituo vinne vya kuchotea maji (vituo viwili katika kila kijiji), ikiwemo ufungaji wa mifumo ya nishati ya jua (solar) kwenye visima vyote viwili.


Naibu Waziri Kundo, aliipongeza Mamlaka ya Maji Mijini na Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Mbozi kwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo na jitihada za kuhakikisha unakamilika kwa wakati.

Aidha, aliwashukuru wananchi wa vijiji vya Ileya na Sambewe kwa ushirikiano wao katika utekelezaji wa mradi huo.

“Ninatoa pongezi kwa Mheshimiwa Mbunge George Mwenisongole kwa juhudi zake kubwa katika kuhakikisha huduma za maji zinapatikana kwa wananchi wa Jimbo la Mbozi...Sasa ni jukumu letu wote kama serikali na jamii kuhakikisha miundombinu ya maji inalindwa na vyanzo vya maji vinahifadhiwa,” alisema Mhandisi Kundo.

Wananchi waliohudhuria hafla hiyo walitoa shukrani za dhati kwa serikali, Mbunge, na washirika wake kwa kujitahidi kutatua changamoto za maji ambazo zilikuwa kero kwa muda mrefu.

Awali katika taarifa yake,Meneja wa  RUWASA Wilaya ya Mbozi, Ismail Nassor, alisema

Miradi hiyo ya maji itahudumia wakazi 4,068 wa vijiji vya Ileya na Sambewe.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI