Header Ads Widget

KESI YA MAUAJI YA KATIBU CCM KILOLO KUENDELEA KESHO ,CCM MKOA WA IRINGA YALAANI VITENDO VYA UKATILI

 

Na Matukio Daima media 

Wakati kesho jumanne  katika Mahakama ya wilaya ya Iringa Kesi ya watuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa katibu wa CCM wilaya ya Kilolo Christina Nindi Kibiki itaendelea ,CHAMA Cha mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa kimesema kinalaani kwa nguvu zote vitendo vya ukatili wa Kijinsia wa aina yoyote Ile na yeyote anayehusika na vitendo vya ukatili achukuliwe hatua Kali za kisheria.


Kauli ya CCM mkoa wa Iringa imekuja ikiwa ni miezi miwili sasa toka katibu wa CCM wilaya ya Kilolo Christina Nindi Kibiki kuuawa kwa kupigwa risasi na Kauli ambayo imekuja baada ya Siku tatu toka watuhumiwa wa mauaji hayo kufikishwa Mahakamani akiwemo diwani wa kata ya Nyanzwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi CCM wilaya ya Kilolo na wengine watatu .

Akijibu swali la waandishi wa habari mkoa wa Iringa juzi Januari 4 mwaka huu wakati wa mkutano wa pamoja kati ya viongozi wa CCM mkoa wa Iringa na waandishi wa habari, mwenyekiti wa Chama hicho mkoa Daud Yassin alisema CCM kimekuwa mstari wa Mbele kupinga ukatili wa Kijinsia na hata kwenye ziara ya Mwenyekiti wa Taifa wa UWT Mary Chatanda ndani ya mkoa wa Iringa Kila sehemu amekuwa akikemea vitendo vya ukatili wa Kijinsia.

Hivyo alisema kama Chama kitaendelea kukemea vitendo hivyo vya kikatili ndani ya mkoa bila kugusia sakata la mauaji ya katibu CCM Kilolo alisema ukatili wa Kijinsia haukubaliki .

Huku mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC ) Salim Abri Asas, alisema ukatili mwingine ni ule wa Wazazi na walezi  kutozingatia lishe bora kwa watoto wao kama njia muhimu ya kuwalinda dhidi ya matatizo ya udumavu na utapiamlo, ambayo yanaathiri maendeleo yao ya kimwili na kiakili.

Alisema kuwa lishe bora ni nguzo muhimu katika kuimarisha makuzi na afya ya mtoto na kuwaandaa kwa ajili ya maisha bora ya baadaye. 

Kuwa changamoto ya udumavu na utapiamlo bado ni tatizo kubwa katika jamii, hivyo ni muhimu kwa wazazi kuhakikisha wanawapa watoto wao mlo kamili unaojumuisha virutubisho muhimu kwa ukuaji wao.

Mnec Asas alisema kuwa ni jukumu la kila mzazi na mlezi kuhakikisha watoto wanapata lishe bora tangu wakiwa watoto wadogo, ili waweze kukuza miili na akili zao na kuwa na nguvu za kupambana na changamoto mbalimbali za maisha.

Pia alisema upo   umuhimu wa kutoa elimu kwa jamii kuhusu lishe bora, ikiwa ni pamoja na matumizi ya vyakula vinavyopatikana kwa urahisi, ili watoto waweze kujikinga na magonjwa na kuwa na afya njema kwa ujumla.


Kuhusu Matokeo ya Uchaguzi wa serikali za mitaa uongozi huo wa CCM mkoa wa Iringa umesema kuwa ushindi mkubwa walioupata katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji, na vitongoji umethibitisha mafanikio ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho, ambayo imeleta maendeleo kwa wananchi kuanzia ngazi ya chini. 

 Mwentekiti wa CCM mkoa wa Iringa Yassin alisema kuwa chama hicho kilijipanga vizuri, na hakikuwa na mpango wa kushinda kwa bahati, kama baadhi ya watu wanavyodhani, bali ilikuwa ni matokeo ya utekelezaji wa sera bora za maendeleo na ushirikiano wa karibu na wananchi katika utekelezaji wa ilani ya ccm. 

"CCM Mkoa wa Iringa iliweza kushinda kwa asilimia 99.99 kwa sababu kilijipanga kuanzia ngazi ya mabalozi na kufanya kazi kwa karibu na wananchi, jambo ambayo limeleta imani kubwa kwa wapiga kura," alisema Yassin. 

Pia, Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa chama cha mapinduzi kiliteuwa wagombea wanaokubalika kwa wananchi, ambao walionesha uwezo wa kutatua changamoto za maeneo yao.  

Hata hivyo Yassin alisema kuwa chama cha mapinduzi mkoa wa Iringa, kimejipanga kuzungumza na viongozi wote waliochaguliwa katika ngazi za mitaa, vijiji, na vitongoji ili kuwakumbusha majukumu yao na kuwahimiza kutekeleza ilani ya chama hicho kwa ajili ya maendeleo endelevu ya wananchi. 

"Hatua inayofuata ni kukutana  na viongozi wote walio chaguliwa ili kuzungumza nao, kuwakumbusha ilani ya CCM na kuhakikisha kuwa wanatekeleza ahadi walizoziweka kwa wananchi kwa maendeleo ya mkoa wetu. 

Alisema Matokeo mazuri ya Uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka Jana ni majibu ya kazi nzuri inayofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na majibu kama haya yatapatikana kwenye Uchaguzi mkuu mwaka huu Uchaguzi wa madiwani ,Wabunge na Rais ambapo kwa mkoa wa Iringa Upande wa Rais hakuna ubishi Samia atashinda kwa Kishindo .

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI