Hamida Ramadhani,
Matukio Daima App Dodoma.
WAZIRI wa Katiba na Sheria,Dk Damas Ndumbaro amesema kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aids Compain (MSLAC) wamebaini wananchi bado wanachangamoto za kisheria katika mambo manne ambayo ni ukatili wa kijinsia,migogoro ya ardhi, ndoa na ardhi.
Kauli hiyo ameitoa leo Jumatatu,Januari 20,2025 wakati akizungumza na Waandishi kuhusiana na kampeni ya Mama Samia Legal Aids Compain (MSLAC) katika mikoa 6 ambayo inatarajiwa kuanza Januari 24 mwaka huu.
Waziri Ndumbaro amesema kupitia kampeni hiyo walifika katika mikoa 11 na changamoto zilizojitokeza kwa wingi ni ukatili wa kijinsia,migogoro ya ardhi, ndoa na ardhi.
Amesema kwenye sekta ya ardhi wamebaini ubabaishaji ni mwingi ambapo amemwomba Waziri wa Ardhi,Deogratius Ndejembi kumtumia orodha ya migogoro sugu ili baada ya kampeni hiyo waanze kuishughulikia.
"Katika sera yetu ya utoaji haki tutahakikisha wananchi wanapata haki na wanapata elimu ya kisheria,"amesema Waziri Ndumbaro.
Amesema waliopo vijijini wana kiu ya haki ndio maana Rais aliunda Tume ya Haki jinai ambayo ilibainisha umuhimu wa haki kumfikia Mwananchi.
Amesema kupitia kampeni hiyo waliweza kuwafikia watu 175,119 ambapo asilimia 49 ni wanawake na 51 ni wanaume ambapo walitatua jumla ya migogoro 3162
"Hizi takwimu wanaume ni wengi kuliko wanawake ni takwimu nzuri tu,unaona Mpango huu unamsaidia Mwananchi kuzalisha zaidi na programu hii ni mkombozi kwa wanyonge hasa wale ambao hawana uwezo wa kupata mawakili,"amesema Waziri Ndumbaro
Amesema Mpango huo unamsaidia mnyonge kupunguza malalamiko katika sekta ya sheria.
Aidha amesema Januari 24 mwaka huu watazindua kampeni hiyo kwa mikoa 6 Mkoani Kigoma.
Ameitaja mikoa mingine watakayofika ni,Kilimanjaro,Geita,Katavi,Tabora na Mtwara,
"Katika mikoa hiyo tutakuwa Januari tu na katika Kila Halmashauri wataenda Kata 10 katika Kila Kata watatumia siku 9 na huduma zitatolewa bure kwa wananchi,"amesema
Amesema wataanzia Januari 24 mkoani Kigoma kisha Katavi,Tabora na Mtwara ambapo Januari 25 watakuwa Geita na Januari 29 watamalizia Kilimanjaro.
Waziri Ndumbaro amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi ili waweze kupata msaada wa kisheria.
0 Comments