HALMASHAURI ya Wilaya ya Kibaha itashirikiana na Mtandao wa Kuwajengea Uwezo Wanawake Tanzania (TAWEN) kuhakikisha wajasiriamali wanapata mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri ambapo kuna kiasi cha shilingi milioni 900.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Regina Biyeda wakati wa mafunzo ya nishati safi ya kupikia kwa wanamtandao hao yaliyofanyika Mlandizi Kibaha
Biyeda amesema kuwa fedha hizo zipo kwa ajili ya makundi ya Wanawake ambao wametengewa asilimia nne , Vijana asilimia nne na Watu wenye Ulemavu asilimia mbili.
"Fedha zipo za kutosha makundi haya yanatakiwa kuchangamkia fursa hiyo ya mikopo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za kiuchumi baada ya mikopo hiyo kusitishwa na sasa imerejeshwa tena,"amesema Biyeda
Kwa upande wake mkurugenzi wa Tawen Florence Masunga amesema kuwa malengo ni kuwafikia wanawake na vijana wasiopungua 10,000 kwa Mkoa wa Pwani na pia kukopesha majiko zaidi ya 3,000 ya nishati safi ya umeme ambapo kwa siku nzima mtu anatumia kiasi cha shilingi 1,000 tu.
Mmojawapo wa wanufaika wa Tawen Suzan Mrema amesema kuwa amefanikiwa kufanyabiashara hadi nje ya nchi na kufanyabiashara kwenye masoko ya kimataifa
0 Comments