Na Fadhili Abdallah,Kigoma
SHIRIKA la maendeleo la serikali ya Ubelgiji (ENABEL) limekabidhi kwa serikali ya mkoa Kigoma mradi wa maji uliokuwa ukitekelezwa katika kijiji cha Mwayaya wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma baada ya mradi huo kukamilika na kuanza kutoa huduma.
Makabidhiano hayo yamefanyika mkoani Kigoma ambapo Balozi wa serikali ya Ubelgiji nchini. Peter Hugyhbaert aliwakilisha serikali ya nchi hiyo katika makabidhiano hayo huku serikali ya Tanzania ikiongozwa na Mkuu wa wilaya Kigoma,Rashid Chuachua kwa niaba ya Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye.
Akizungumza katika makabidhiano hayo Balozi Hugyhbaert alisema kuwa kutekelezwa kwa mradi huo kwa ufadhili wa serikali ya Ubelgiji kupitia Shirika la ENABEL kutokana na mahusiano ya kindugu na muda mrefu yaliyopo baina ya serikali ya nchi hiyo na Tanzania hasa katika kusaidia mahitaji ya kibinadamu ya wananchi wa vijijini.
Naye Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la ENABEL nchini, Koenraad Goekint akizungumza katika makabidhiano hayo amesema kuwa serikali ya Ubelgiji kupitia ENABEL imetekeleza mradi huo baada ya kuona mahangaiko ya wananchi hao wa Kigoma ambapo wanawake na Watoto walikuwa wakihangaika kufuata maji umbali mrefu jambo lililokuwa likisababisha wanafunzi kukosa masomo na wanawake kushindwa kufanya shughuli za kiuchumi za kuwaingizia kipato.
Akipokea mradi huo kwa niaba ya serikali ya mkoa Kigoma Mkuu wa wilaya Kigoma,Rashid Chuachua akimwakilisha Mkuu wa mkoa Kigoma ameishukuru serikali ya Ubelgiji na Shirika la ENABEL kwa kufanikisha utekelezaji wa mradi huo ambao unawezesha watu 15,000 kupata maji safi na salama na kuondoa changamoto kubwa ya wananchi wa Kijiji hicho cha Mwayaya kuhangaika kutafuta maji safi na salama.
Chuachua ameishukuru ENABEL akieleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo ambao ni sehemu ya miradi saba ya maji yenye thamani ya shilingi Bilioni 18 inayotekelezwa na shirika hilo mkoani Kigoma na kwamba miradi hiyo inadhihirisha uwepo wa mshikamano na urafiki baina ya nchi hizo mbili.
0 Comments