Header Ads Widget

CHAMA CHA SOKA IRINGA CHAPONGEZA WADAU WOTE KWA KUCHANGIA MICHEZO MWAKA 2024


Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa, Cyprian Kuyava, ametoa pongezi kwa wadau wote waliowekeza katika maendeleo ya michezo ndani ya mkoa huo mwaka 2024. Akizungumza na vyombo vya habari, Kuyava alisema kuwa juhudi za wadau mbalimbali zimekuwa chachu ya maendeleo ya michezo, hususan soka, katika mkoa wa Iringa, licha ya changamoto zilizopo.

Kuyava akizungumza na Matukio Daima media alieleza kuwa jitihada za chama hicho ni kuhakikisha mkoa wa Iringa unarejea kwenye ligi kuu ya Tanzania Bara.

 “Iringa ni mkoa wenye historia kubwa ya michezo, na tunapambana kuhakikisha tunarudisha hadhi yetu ya kimichezo. Hili halitawezekana bila juhudi za pamoja za wadau wa michezo, serikali, na vyombo vya habari,” alisema Kuyava.


Mwenyekiti huyo alitambua mchango wa wadau mbalimbali waliojitolea kuhakikisha mkoa wa Iringa unasonga mbele katika michezo. 

Aliwataja baadhi ya wadau wakubwa akianza na Kampuni ya Asas, chini ya uongozi wa Mkurugenzi Salim Abri Asas. Kuyava alisifu jitihada za Salim Abri Asas kwa kuwa mdau mkubwa wa michezo na msaidizi wa muda mrefu katika maendeleo ya soka la mkoa wa Iringa.

“Kampuni ya Asas imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia soka la Iringa. Mkurugenzi wake hajawahi kuchoka kutuunga mkono kwa hali na mali. Michango yake inapaswa kuwa mfano kwa wadau wengine,” aliongeza.

Wadau wengine waliosifiwa ni uongozi wa serikali ya mkoa wa Iringa pamoja na ofisi ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada pamoja na Feisal Abri Asas ambae pia mchango wake ni mkubwa sana pia wapo wabunge na viongozi wengine wa kisiasa .

Kuyava alitoa pongezi kwa juhudi zao za kuhakikisha miundombinu ya michezo, ikiwemo Uwanja wa Samora, inaboreshwa na kuwa katika hali bora.

Aliendelea kumpongeza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daud Yassin, kwa kushirikiana na chama chake katika kutoa mchango wa maendeleo ya michezo.

 Alieleza kuwa viongozi hao wamekuwa wakifanya kazi bega kwa bega na chama cha mpira wa miguu kuhakikisha mkoa unarudi katika ramani ya soka kitaifa.

Mbali na viongozi wa taasisi, Kuyava alitambua mchango wa makundi mbalimbali ya mitandao ya kijamii kama WhatsApp. Makundi hayo yamekuwa yakihamasisha michango ya kifedha na mali kwa ajili ya maendeleo ya michezo.

 Aidha, alitoa shukrani kwa watu binafsi waliokuwa tayari kusaidia juhudi za kurejesha hadhi ya michezo mkoani Iringa.

“Mchango wa kila mmoja, iwe ni mtu binafsi au kupitia makundi, umekuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya soka letu.

 Tunapenda kusema asante kwa kila mmoja aliyeshiriki kwa njia yoyote,” alisema Kuyava.

Kuyava pia aliwapongeza wanahabari wa mkoa wa Iringa kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuendeleza michezo. Alieleza kuwa vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika kuhamasisha na kufanikisha maendeleo ya michezo mkoani.

“Vyombo vya habari vimekuwa sauti ya michezo mkoani Iringa. Wanahabari hawachoki kuripoti na kuhamasisha wananchi kujitokeza kuunga mkono michezo. Tunawaomba waendelee na kazi hii nzuri kwa sababu inasaidia kuleta mshikamano na maendeleo,” alisema Mwenyekiti huyo.

Kuyava alisisitiza kuwa ili mkoa wa Iringa urejee kwenye ligi kuu, ni muhimu wadau wote kushirikiana bila kunyosheana vidole. Alitoa wito kwa kila mdau kuona ana mchango muhimu katika juhudi hizi na kuungana kwa lengo moja—kurejesha hadhi ya michezo ya mkoa wa Iringa.

“Tunapasa kusimama pamoja bila kujali tofauti zetu. Hili ni jukumu la kila mmoja wetu. 

Hakuna haja ya kulaumiana; badala yake, tushirikiane na kutumia fursa tulizonazo kwa faida ya michezo ya Iringa,” alisisitiza.

Pamoja na pongezi hizo, Kuyava hakusita kuzungumzia changamoto zinazoikabili michezo mkoani Iringa. Alitaja ukosefu wa rasilimali za kutosha na changamoto za kifedha kama baadhi ya vikwazo vinavyosababisha maendeleo ya polepole.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa changamoto hizi hazipaswi kuzuia juhudi za maendeleo. Alitoa wito kwa wadau zaidi kujitokeza kusaidia kwa hali na mali ili kuziba pengo la rasilimali na kuhakikisha lengo la kurejesha ligi kuu linafanikiwa.

Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa, Cyprian Kuyava, aliwataka wadau wote kuendelea kushirikiana na chama chake katika kuimarisha michezo mkoani. 

Alisema kuwa kwa umoja na mshikamano, mkoa wa Iringa utaweza kurejesha hadhi yake ya kimichezo na hata kuvuka matarajio ya wengi.

“Ni lazima tuchukue hatua sasa ili kufanikisha ndoto zetu. Soka ni zaidi ya mchezo ni chanzo cha mshikamano na maendeleo ya jamii. Tunawaomba wadau wote, kutoka sekta binafsi, serikali, na jamii kwa ujumla, kuungana nasi katika juhudi hizi,” alihitimisha Kuyava.

Chama Cha soka mkoa wa Iringa kitaendelea kuheshimu mchango wa Kila mmoja Wetu katika kuendelea michezo ndani ya mkoa na haitakubali kuona wadau hao wakivunjwa moyo kwa namna yoyote Ile .


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI