Header Ads Widget

ATHARI MABADILIKO YA TABIA NCHI KWA WATOTO, VIJANA DODOMA

Na Hamida Ramadhan ,Matukio Daima

Ripoti ya ‘Hali ya Watoto Duniani 2024’ iliyotolewa na Shirika la Watoto Ulimwenguni (Unicef) inabashiri kutokea kwa athari kubwa na za pande nyingi za mabadiliko ya tabianchi na ya mazingira, ambazo zinaweza kuwaingiza watoto katika nyakati ngumu za kimalezi na makuzi yao.


The ‘State of the World’s Children 2024: The Future of Childhood in a Changing Worl ni ripoti ya UNICEF inayojadili kwa kina mustakabali wa utoto katika Dunia Inayobadilika, ikichunguza pamoja na masuala kadhaa yenye mweleleo wa kuthiri maisha ya watoto ifikapo mwaka 2050, huku suala la majanga ya hali ya hewa na mazingira likiwa mojawapo.


Miongoni mwa athari zinazotajwa na ripoti hiyo ni pamoja na ongezeko la hatari za kiafya kwa makuzi ya watoto kwani uchafuzi wa hewa unaathiri afya ya mfumo wa upumuaji, huku matukio ya hali mbaya ya hewa yakitajwa kusababisha kuenea kwa magonjwa kama malaria, dengue, na zika kupitia ongezeko la mbu.

Magonjwa yanayoenezwa kwa maji: Mafuriko yanayosababishwa na kuongezeka kwa kina cha bahari na hali mbaya ya hewa huchafua vyanzo vya maji, na kusababisha magonjwa ya kuhara—ambayo ni chanzo kikuu cha vifo kwa watoto chini ya miaka mitano,” insomuch sehemu ya ripoti hiyo iliyotolewa Novemba 2024.

Athari hizo za mabadiliko ya tabianchi na nyingine zinazotajwa katika ripoti hiyo, zinashabihiana na zile zinazotajwa kuwapo mkoani Dodoma na kusababisha madhara kwa kundi la watoto na vijana wa Mkoa huo.

Ripoti ya lishe ya mkoa huo inabainiha kuwa Dodoma hupokea mvua mara moja tu kwa mwaka, hali ambayo huathiri lishe, afya, elimu, na maendeleo ya watoto kwa ujumla, huku jamii ikikabiliana na changamoto za kiuchumi na kijamii zinazozidi kuwaathiri kwa kiwango kikubwa.


Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ukosefu wa mvua umeathiri kilimo cha mazao tegemezi kama mahindi, mtama na mihogo, hali iliyosababisha upungufu wa chakula. 

Ukosefu wa chakula umesababisha ongezeko la utapiamlo, hasa kwa watoto, ambapo tafiti zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 30 ya watoto wa Dodoma wanakabiliwa na udumavu kutokana na lishe duni.

“Tafiti za kidemografia za mwaka 2022 zinaonesha udumavu miongoni mwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano umepungua kutoka asilimia 37 mwaka 2015/2016 hadi asilimia 30, lakini bado hali si nzuri,” anasema Senyamule.

Ukosefu wa chakula, pia ni athari inayotajwa na ripoti ya UNICEF ya Hali ya Watoto Duniani 2024 ikisema: “Mabadiliko yasiyotabirika ya hali ya hewa yanavuruga uzalishaji wa chakula, hivyo kuongeza utapia mlo na njaa miongoni mwa watoto, hali inayoweza kuathiri ukuaji wa mwili na akili”.

Ripoti ya UNICEF inasema majanga yanayosababishwa na hali ya hewa kama mafuriko na vimbunga yamesababisha kufungwa na kuharibiwa kwa miundombinu ya elimu. Kwa mfano, tangu mwaka 2022, wanafunzi milioni 400 duniani wamekumbana na usumbufu wa shule kutokana na matukio makali ya hali ya hewa.


Mkoani Dodoma, ukame unaoendelea unatajwa kusababisha ukosefu wa maji safi na salama, hali ambayo imechangia ongezeko la magonjwa kama kipindupindu, kuhara, na magonjwa ya ngozi, yanayowaathiri zaidi watoto. 


Wanakijiji wengi katika maeneo ya Bahi Sokoni wanategemea maji kutoka mabwawa ya asili au visima vya muda ambavyo mara nyingi si salama kwa matumizi.


Mariam Zakaria ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Bahia Sokoni, anasema kuwa watoto wengi wanakosa nguvu za kusoma kutokana na njaa na magonjwa yanayosababishwa na lishe duni. 


“Hali ya ukame imewalazimisha baadhi ya wanafunzi kutega shule ili kwenda kufanya kazi za muda kama kuchota maji au kuuza bidhaa ndogo ndogo mitaani ili kusaidia familia zao,” anasema Zakaria.

Esther Mazoea mbaye ni mwanafunzi wa darasa la saba, anaeleza jinsi changamoto ya ukosefu wa chakula inavyoathiri masomo yao. “Tunashindwa kusoma vizuri kwa sababu tunakosa nguvu ya chakula. Hali hii inaturudisha nyuma na kufanya ndoto zetu ziwe ngumu kufikiwa,” anasema Mazoea.

Stella Kimambo, Ofisa Lishe wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), yeye anaetoa wito kwa Watanzania kuzingatia mwongozo wa chakula na ulaji uliozinduliwa na serikali ili kuboresha afya zao. 


“Badala ya kutumia Google kutafuta maelekezo ya lishe bora, jamii inapaswa kufuata mwongozo wa serikali, ambao umebainisha vyakula vyenye virutubishi vinavyohitajika na mwili kulingana na mazingira yao,” alisema Kimambo.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe katika Wizara ya Afya, Neema Mwapili, alisema serikali imeendelea kuboresha afua za lishe, huku ikisisitiza kuwa chakula cha shule kinapaswa kuwa na mchanganyiko wa virutubishi muhimu.

 

“Chakula kinachotolewa shuleni lazima kiwe na uwiano mzuri wa virutubishi. Wanafunzi hawapaswi kula wali na maharage kila siku; lazima pawe na nyongeza ya madini muhimu kama madini joto,” alisema Mwapili.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Kaspar Mmuya, amewataka wadau wa lishe kuelimisha jamii kuhusu athari za kula chakula cha aina moja.

“Tunahitaji kubadilisha mitazamo ya watu, hasa katika vijiji, kuhusu lishe. Watu wengi wanaamini kwenye chakula kimoja tu, lakini tunapaswa kuwaelimisha umuhimu wa kula mlo mchanganyiko kwa afya bora,” alisema Mmuya.

Wakati Ripoti ya ‘Hali ya Watoto Duniani 2024 inapendekeza Ripoti haja ya kuchukua hatua za haraka zenye kuwalenga watoto katika kukabiliana na mgogoro wa tabianchi ambazo ni pamoja na kupunguza uzalishaji wa kaboni na kuwekeza katika vyanzo vya nishati endelevu ikiwa ni hatua ya kupunguza athari za muda mrefu za mabadiliko ya tabianchi kwa watoto.

Pendekezo jingine katika ripoti hiyo ni: “Serikali zinapaswa kuzingatia uimara wa miundombinu, upatikanaji wa maji safi, na maandalizi ya majanga katika shule na mifumo ya afya, kipaumbele kinapaswa kutolewa kwa maeneo yenye hatari kubwa na makundi yaliyo hatarini ili kupunguza tofauti na kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa nyuma.”

Kadhalika ripoti hiyo inasisitiza umuhimu ushirikishaji wa vijana katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha sauti za watoto zinasikika katika mijadala ya suala hillo, ushiriki wenye lengo la kuhakikisha haki yao ya kuthibitisha kuwa sera zinazotungwa zinaakisi mahitaji na matarajio yao.

Kati ya Septemba na Oktoba 2024 wakiwa sehemu ya mamia ya watoto na vijana kutoka mataifa 20, walioshiriki mikutano ya utangulizi kabla ya kusanyiko la kimataifa la Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP29) uliofanyika Baku, Azerbaijan, watoto wa Tanzania walitoa mapendekezo kadhaa likiwamo linayitaka serikali kuwashirikisha katika masuala yanayohusu mabadiliko ya tabianchi.

Nchini Tanzania Shirika la WeWorld linaendesha miradi ya uhifadhi ya mazingira katika mikoa ya Dar es Salaam na Njombe ikiwahushirikisha wanafunzi katika baadhi ya shule za msingi ikiwa ni hatua ya kuhakikisha vijana na watoto wanashiriki katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.

Kupitia kazi za WeWorld kwenye utekelezaji wa miardi ya 'PAMOJA TUNABORESHA ELIMU' katika baadhi ya shule za msingi za Dar es Saalaam, na ile ya KITE na MAMMIE katika mikoa wa Njombe, ni mfano hai unaojibu kiu ya maazimio mengi ya makundi ya vijana na watoto wanaopaza sauti wakidai ushiriki kamili katika masuala yahusuyo tabianchi.

Mfano halisi ni ule unaopatikana katika Shule ya Msingi ya Kawe, Manispaa ya Kinondoni ambako kwa kushirikiana na We World, shule hiyo, imeanzisha Klabu ya Wakulima Chipukizi, ambako watoto wanafundishwa kulima mboga kama mchicha, nyanya, na maboga.

Kwa mujibu wa Tovuti ya IPP kilimo hicho huchangia siyo tu lishe bora, bali pia huimarisha afya zao kwa kupunguza uwezekano wa kushambuliwa na magonjwa yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi kama pumu na saratani ya ngozi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, tayari miti 60 imepandwa kuzunguka maeneo ya shule, ikiwa ni hatua ya kupunguza ukame na kuhifadhi uoto wa asili.

Lengo la shule hiyo ni kupanda miti 50 zaidi, hasa ya matunda, ili kuhakikisha wanafunzi wanapata kivuli na lishe bora, kupitia juhudi hizo, watoto wanajifunza umuhimu wa mazingira na jinsi ya kuyatunza.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI