Header Ads Widget

WAZIRI SIMBACHAWENE ATOA WITO KWA WATANZANIA KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA

 Na Hamida Ramadhan Matukio Daima App Mpwapwa

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na  Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, George Simbachawene  ametoa wito kwa Watanzania wenye sifa za kujiandikisha katika Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kujitokeza kwa wingi  katika vituo ili kupata Kitambulisho cha Mpiga Kura kitakachowawezesha kupata haki ya kuchagua Viongozi katika Uchaguzi Mkuu ujao .

Pia,  Waziri Simbachawene amewataka Watumishi wa Umma nchini kuhakikisha wanatumia haki yao  kujiandikisha kwenye daftari hilo ili kuwawezesha kuchagua viongozi akiwemo Rais, Wabunge pamoja na Madiwani  kwenye uchaguzi huo .

Waziri Simbachawene ametoa wito huo leo Jumatatu  Desemba 30, 2024 mara baada ya kuboresha taarifa zake kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Kituo cha Wapiga Kura kilichopo Kata ya Pwaga  Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma.

Amesema kitendo cha kwenda kuboresha taarifa katika kituo husika kwa Mtumishi wa Umma ni kujihakikishia usahihi wa taarifa zake pamoja na uhakika wa mahali atakapopigia kura.

“ Nimefika hapa ndani ya muda mfupi nimeboresha taarifa zangu ambapo nimepata kitambulisho kipya  kitakachoniwezesha kutumia haki yangu ya kidemokrasia muda utakapowadia wa

kuchagua na kuchaguliwa ”, amesema Waziri Simbachawene.

Katika hatua nyingine Waziri Simbachawene  ameipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuboresha zoezi hilo na kufanya kazi kwa weledi inayoimarisha Demokrasia nchini huku akisifu jinsi zoezi hilo linavyoendesha kwa umakini na uharaka ili kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zingine za kujiingizia kipato 

Aidha, Waziri Simbachawene  amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa kuendelea kuimarisha Demokrasia nchini na kuendelea kuiwezesha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Awali, Mwandikishaji wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Kituo hicho  Christina Chigohe ameeleza kuwa zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linafanyika kwa siku saba ambapo lilianza Desemba 27 na litafikia tamati Januari 3, 2025.


Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaoendelea unaongozwa na kaulimbiu “Kujiandikisha kuwa Mpiga Kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora”.





 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI