WAANDISHI wa habari nchini wamepongezwa kwa kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili ndani ya jamii.
Hayo yamesemwa na Edna Kataraiya kutoka Ofisi ya Mipango na Uratibu Mkoa wa Pwani wakati wa kuhitimisha siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili kimkoa zimefanyika Kwa Mbonde Wilayani Kibaha.
Kataraiya amesema waandishi wa habari wamesaidia kufichua vitendo vya ukatili na kutoa elimu ya kupinga vitendo hivyo.
Amesema kuwa matukio ya vitendo vya ukatili Mkoa wa Pwani yamepungua kwa asilimia 19.3 kwa mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana.
"Matukio hayo yamepungua kutoka matukio 8,573 mwaka 2023 na kufikia matukio 6,916 mwaka huu,"amesema Kataraiya
Kwa upande wake Polisi Kata ya ya Picha ya Ndege Ibrahim Makaruti amesema kuwa moja ya changamoto inayojitokeza ni baadhi ya wazazi kumalizana nyumbani pasipo kuyapeleka kwenye vyombo vya sheria.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu Wenye Ulamavu Tanzania (SHIVYAWATA) Kibaha Mjni Jabir Makasala alisema kuwa kutungwe sera ya kuwakopesha wazazi wenye watoto wenye ulemavu ili wafanye shughuli za ujasiriamali kwani wazazi hao hawana kipato chochote.
Naye Mkurugenzi wa African Talent Forum (ATF) Rosemery Bujash amesema kuwa wamekuwa wakitoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili kwa vijana wa makundi mbalimbali kupitia sanaa na michezo.
Akitoa salamu za taasisi ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mariam Mnengwah amesema kuwa wao walitoa elimu iliyosaidia kuibua vitendo vya ukatili na kutoa msaada wa kisheria na msaada wa matibabu.
0 Comments