NA MATUKIO DAIMA MEDIA,IRINGA
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa ya Kikristo Tanzania (CCT) Mkoa wa Iringa, ambaye pia ni Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Dkt. Blaston Gaville, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na miradi ya kimkakati.
Akitoa salamu za Krismasi mara baada ya ibada ya kitaifa ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa la KKKT Dayosisi ya Iringa, Dkt. Gaville alisema CCT na waumini kwa ujumla wanaipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayofanyika, zinazoonekana na hata zile zisizoonekana kwa macho ya kawaida.
Alieleza kuwa miradi mikubwa ya kimkakati kama ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na uendelezaji wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Julius Nyerere ni mfano mzuri wa juhudi hizo. Pia, aliipongeza Serikali kwa kuzindua vifurushi vipya vya bima ya afya kwa makundi mbalimbali, hatua inayolenga kuboresha afya za Watanzania wengi.
“Watanzania wenzangu, huu ni wakati wa kumuombea Rais wetu na Serikali yake kwa ujumla. Utekelezaji huu wa miradi tunaouona haujafanyika kwa muda mrefu nchini. Hii ni fursa ya kuimarisha maendeleo na afya ya wananchi wetu,” alisema Askofu Dkt. Gaville.
Alisisitiza umuhimu wa kulinda na kutunza miradi hiyo, huku akiwataka wakristo na Watanzania kwa ujumla kutambua mchango wa Serikali katika kukuza sekta za elimu, afya, na uwekezaji wa kimkakati.
Aidha, aliwapongeza Watanzania wote walioshiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa amani, akiwahimiza wale waliokosa nafasi za uongozi kushirikiana na viongozi waliochaguliwa ili kudumisha amani na maendeleo ya taifa.
Dkt. Gaville pia aliwakumbusha Watanzania juu ya changamoto za hali ya hewa, akiwataka wakulima kutumia mbegu zinazostahimili ukame na wananchi wote kutunza vipato vyao badala ya kuendekeza matumizi yasiyo ya lazima.
Mgeni maalum katika ibada hiyo, Mbunge wa Jimbo la Iringa Jesca Msambatavangu, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Iringa, aliwahimiza waumini kuishi kwa mujibu wa maandiko matakatifu ili kukabiliana na changamoto za kidunia.
Alisema kila mtu anapochukua nafasi yake kikamilifu katika familia na jamii, matatizo mengi yanayowakabili vijana kama ukatili wa kijinsia na mmomonyoko wa maadili yanaweza kuepukwa.
Askofu Mstaafu wa KKKT, Dkt. Owdenburg Mdegela, alizungumzia changamoto za kijamii zinazoukabili Mkoa wa Iringa, zikiwemo matendo ya ukatili, udumavu, na maambukizi ya UKIMWI. Alisisitiza kuwa wazazi wana jukumu la kukemea na kuripoti vitendo vya ukatili dhidi ya watoto badala ya kuficha wahalifu.
Alisema kuwa hali ya usafiri wa wabunge inapaswa kuboreshwa, akipendekeza utaratibu wa kusafiri kwa magari tofauti au hata usafiri wa anga ili kuepuka ajali za mara kwa mara zinazolitia doa Taifa.
Ibada ya kitaifa ya Krismasi mkoani Iringa, iliyofanyika katika Kanisa la KKKT Dayosisi ya Iringa, ilitanguliwa na mkesha wa Krismasi katika Kanisa Kuu la Romani Katoliki Jimbo la Iringa, ulioshirikisha viongozi mbalimbali wa dini kutoka ndani na nje ya nchi. Viongozi hao walisisitiza mshikamano, maadili, na uzingatiaji wa maandiko kwa ustawi wa taifa.
0 Comments