Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Zaidi ya shilingi Trilioni 3.4 zinapaswa kukusanywa kwa wafanyabiashara yakiwa ni malengo ya Mamlaka ya mapato Tanzania TRA nchini ili ziende kutekeleza miradi ya maendeleo kwa maslahi mapana ya Taifa.
Mkurugenzi wa elimu kwa mlipa kodi TRA Nchini Richard Kayombo akiwa mkoani Njombe amewaambia wafanyabiashara kuwa hakuna namna nyingine ya kutekeleza miradi ya maendeleo zaidi ya kukusanya fedha hizo ambazo zitasaidia Taifa kufanya maendeleo.
Aidha Kayombo amesema Fedha hizo zinapaswa kukusanywa toka kwa wafanyabiashara bila vurugu na hii itasaidia kushughulikia changamoto za miundombinu zikiwemo za barabara,Maji,Elimu pamoja na Afya.
Lusungu Mbede ni Ofisa biashara mkoa wa Njombe ambaye anasema wapo tayari kushughulikia changamoto zozote zinazowakwamisha wafanyabiashara ili waweze kulipa kodi kwa hiari na kwa moyo mkunjufu.
Awali Meneja wa mamlaka ya mapato Tanzania TRA Specioza Owure amesema mkoa wa Njombe umefanikiwa kuvuka lengo la makusanyo na kuwa na ziada ya zaidi ya shilingi milioni 600.
Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara mkoani Njombe akiwemo Sifael Msigala mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanyabiashara mkoa wa Njombe,Humphrey Millinga,Anjelus Nziku na Padre Salvatory Ngimbudzi wameiomba serikali kushughulikia changamoto ya kodi nyingi kwenye biashara moja kwani zimekuwa kikwazo kikubwa kwao.Wamesema Kodi zikipungua inaweza kusaidia wawekezaji kuongeza uwekezaji vikiwemo viwanda kwani Mkoa wa Njombe bado una viwanda vichache.
0 Comments