Header Ads Widget

THRDC WAMPAMBANIA WAKILI LUSAKO KUPATA MALI ZAKE POLISI


Wakili Msomi Alphonce Lusako, siku ya Jumanne Desemba 17, 2024, amekabidhiwa vifaa vyake ikiwemo gari na kompyuta mpakato (laptop) vilivyochukuliwa na Jeshi la Polisi, maeneo ya Makumbusho, Dar es Salaam.

Akizungumza Leo Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa, amesema Jeshi la Polisi lilichukua vifaa vya Wakili Lusako kutokana na kumtafuta mtuhumiwa Emmanuel Mweta. Polisi walidai kuwa Mweta alikuwa akitumia gari linalofanana na la Wakili Lusako na siku hiyo alionekana maeneo ya Makumbusho.

Aamesema THRDC iliendelea kufuatilia suala hilo kwa kuhakikisha usalama wa Lusako unaendelea kuwepo na kuendelea kuwasiliana na Jeshi la Polisi kwa ajili ya hatua zingine za kiusalama.


"Tunashukuru Jeshi la Polisi limetupa ushirikiano mkubwa, na leo tumekutana na RPC wa Kinondoni kwa ajili ya kujadili yaliyotokea na kujiridhisha kwamba polisi walikuwa wanamtafuta mtuhumiwa Emmanuel ambaye alikuwa anafanya kazi katika jengo jirani na ofisi za Lusako", ameeleza Olengurumwa.

Aidha ameeleza kuwa mtuhumiwa Emmanuel alikuwa ni mdaiwa aliyetapeli Watanzania kiasi cha pesa (hakijatajwa) ambaye aliruka dhamana baada ya kuwa amekamatwa, ndipo ikawabidi polisi kumtafuta, isivyo bahati wakamdhania Lusako kuwa Emmanuel.

"Mazingira tuliyoyaona ni kwamba hata Bwana Emmanuel siku hiyo alikuwa anatumia gari inayotaka kufanana na ya Lusako na alikuwa katika maeneo ambayo Lusako alikuwa akienda ofisini kwake", ameeleza.

Kwa upande wake, Wakili Lusako amesema kuwa tukio hilo lilimsababisha kukimbia kutokana na hofu aliyokuwa nayo. Ameeleza kuwa kwa sasa hali yake inaendelea kuimarika, ingawa bado ana hofu kutokana na matukio ya mara kwa mara yanayofanana na vitendo vya utekaji.

"Kwa muktadha wa namna taifa letu lilivyo kwa sasa, watu wanatekwa, watu wanapotezwa, kwahiyo nilikuwa na chaguo la kutetea uhai wangu", ameeleza Lusako.

Halikadhalika amewashukuru Watanzania wote walionesha kuguswa na tukio lile kwa kushikamana naye, ikiwamo wanahabari ambao waliweza kuripoti tukio lake, hali ambayo ameieleza kuwa ilimpa amani na kumhakikishia kuwa salama tofauti na iwapo tukio hilo lingekaliwa kimya.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI