Header Ads Widget

MRADI WA FEED THE FUTURE TANZANIA WAWAKABIDHI VIJANA IRINGA VIFAA VYA KILIMO VYA TSH MILIONI 1000



Mkuu wa wilaya ya Iringa Kheri James akimkabidhi jembe la kukokotwa na Ng'ombe mmoja kati ya Vijana wa Mradi wa Feed the Future 

Na Matukio Daima media 

Mradi wa Feed the Future Tanzania kwa kushirikiana na Agriedo Hub umekabidhi vifaa vya kilimo, ufugaji, na usindikaji vyenye thamani ya shilingi milioni 100 kwa vijana 75 huku malengo yakiwa kuwafikia vijana 200 ifikapo Januari 2025.

Meneja wa Mradi wa Feed the Future Tanzania, Mshindi Isaya, alibainisha kuwa lengo kuu la mradi huo ni kuwajengea uwezo vijana walio katika mnyororo wa thamani wa kilimo kwa kuwapatia masoko, huduma za kifedha, na zana zinazoongeza uzalishaji wa mazao yenye tija. 

Isaya alisema mradi huo wa miaka mitano unalenga kusaidia vijana wasiozidi miaka 35 kwa kuwa umri huo una nguvu ya kazi na uwezo wa kuzalisha kwa ufanisi zaidi.

"Kupitia mradi huu, tunawaunganisha vijana na taasisi za kifedha na kuwatafutia masoko, tukiwa na dhamira ya kuona vijana wakifanya kilimo cha kisasa kinachoweza kutatua tatizo la ajira," alisema Isaya.


Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Agriedo Hub, Charles Masasi, alisema vijana walichangia shilingi laki tatu kwa kila kifaa huku mradi ukichangia shilingi laki saba, ambapo kila kijana alipata kifaa chenye thamani ya shilingi milioni moja.

 Vifaa hivyo vilihusisha zana za kilimo, ufugaji, na usindikaji vyenye thamani ya shilingi milioni 100 kwa jumla.

Masasi alieleza kuwa mradi huo ulianzishwa kutatua changamoto za vijana zisizoepukika, kama vile ukosefu wa mtaji na kutoaminika na taasisi za kifedha. 

Vifaa vilivyotolewa vitasaidia vijana kuanza au kuimarisha shughuli zao za kilimo kwa ufanisi zaidi.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James, aliipongeza Feed the Future na Agriedo Hub kwa mchango wao katika maendeleo ya vijana. 

Alitoa wito kwa vijana hao kutumia vifaa walivyopokea kwa ufanisi na kuhakikisha wanavitunza ili viwasaidie kwa muda mrefu.

"Teknolojia hii mpya itawasaidia vijana kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji kisasa, jambo ambalo litazalisha ajira nyingi na kuinua uchumi wa Mkoa wa Iringa," alisema Kheri.


Adija Jaabir, Mwakilishi wa Agriedo Hub, alisema malengo makubwa ya kituo hicho ni kuwasaidia vijana wanaojihusisha na kilimo katika nyanda za juu kusini kwa kuwaunganisha na masoko, mitaji, na elimu ya biashara. 

Aliongeza kuwa asilimia 30 ya gharama ya vifaa vilichangiwa na vijana wenyewe, huku asilimia 70 ikitolewa kupitia ufadhili wa mradi huo.

Mwakilishi wa Wizara ya Kilimo, Vumilia Zikankuba, alisema serikali imekuwa ikitambua kilimo kama fursa kubwa kwa vijana na imejikita kutatua changamoto zinazowakabili kama upatikanaji wa ardhi, mitaji, masoko, na teknolojia. 

Alieleza kuwa serikali kupitia programu ya Jenga Kesho Iliyobora imesaidia kuanzishwa kwa mashamba makubwa ya pamoja, ambapo vijana wanapewa maeneo ya ardhi kwa ajili ya kilimo biashara.


Ayoub Kaguo, mkulima wa mbogamboga wilayani Mufindi, alisema mradi huo umemwezesha kupata mashine ya umwagiliaji ambayo awali hakuweza kuinunua kutokana na changamoto za kifedha.

Alisema mashine hiyo itaboresha uzalishaji wake kwa kurahisisha kazi za umwagiliaji.

Kwa ujumla, mradi wa Feed the Future Tanzania na Agriedo Hub unaendelea kuwa nguzo muhimu katika kutatua changamoto za ajira kwa vijana kupitia uwekezaji katika sekta ya kilimo na mifugo.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI