Balozi wa Tanzania nchini Cuba Humphrey Polepole ametangaza kujiuzulu kwenye nafasi hiyo, akisema hatua hii imetokana na “matukio ya hivi karibuni ya wazi ya kukiuka misingi, utamaduni na desturi za Chama cha Mapinduzi (CCM)”.
Katika barua kwa Rais Samia Suluhu Hassan aliyochapisha katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, Polepole ametilia doa mchakato wa uteuzi wa wagombea ndani ya chama hicho huku taifa hilo likijiandaa kwa uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.
Mbunge huyo wa zamani wa kuteuliwa ambaye pia aliwahi kuhudumu kama balozi wa Tanzania nchini Malawi amesema kauli maarufu ya CCM ya “Chama kwanza mtu baadaye” inafanyika vinginevyo.
“Kwa kuwa siwezi kuendelea kuwa sehemu ya uongozi usiohamasika na utii wa misingi ya Katiba ya nchi na chama, haki, maadili, utu na uwajibikaji wa wananchi, nimeamua kwa hiari yangu kujiuzulu nafasi yangu ya uongozi na utendaji serikalini,” alisema Polepole, akiongeza kuwa ataendelea kuwa mwanachama wa kawaida wa CCM.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makala, amekanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni kuwa baadhi ya makada wa chama hicho wameenguliwa katika hatua za awali za mchakato wa kuwania ridhaa ya kugombea ubunge.
Kuhusu barua ya Polepole amesema kama kweli barua hiyo ni ya kweli basi hayo ni maoni yake binafsi, ni ridhaa yake na mawazo yake na kuwa kama alivyokiri kuwa ataendelea kuwa mwanachama wa CCM, basi anatambulika kuwa mwanachama wa chama hicho.
Humphrey Polepole ni nani?
Humphrey polepole amekuwa mwanasiasa maarufu kwa takriban miaka 10 kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania Malawi mwaka 2022. Alikulia katika Umoja wa Vijana wa CCM.
Alianza kujulikana zaidi mwaka 2012 alipoteuliwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete kuwa mjumbe wa Tume ya Katiba mpya, iliyoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba na kumaliza kazi yake mwaka 2014.
Mwaka 2016 Rais John Magufuli alimteua Polepole kuwa Mkuu wa wilaya ya Musoma, mkoani Mara, alikohudumu kwa miezi michache kisha kuhamishiwa Ubungo Dar es Salaam kwa nafasi hiyo hiyo ya ukuu wa wilaya na kuhudumu kwa miezi michache pia.
Umaarufu wake uliongezeka alipoteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, nafasi ambayo kimsingi ni ya kuwa msemaji wa chama.
Anafahamika kwa kutetea sera na utendaji wa CCM na serikali ya Rais Magufuli, hata pale kulipokuwa na utata mkubwa wa masuala kama vile tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu, utekaji, kuwaweka watuhumiwa mahabusu kwa muda mrefu na wengine kufunguliwa kesi nzito za uhujumu uchumi na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu wa 2020. Rais Samia alipoingia madarakani Machi 2021, Polepole hakukaa kwa muda mrefu kwenye nafasi ya usemaji kwani aliondolewa kisha kuteuliwa kuwa Mbunge kabla ya kuteuliwa balozi nchini Malawi.
Anajulikana pia kwa kauli tata au ahadi za CCM na serikali ambazo hazikuwa kutekelezwa, kama vile ujenzi wa barabara za juu (fly overs) katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Hadi sasa barabara za juu zimejengwa nne katika maeneo ya Ubungo, Tazara, Chang'ombe na makutano ya barabara za Mandela na Kilwa.
Wakati fulani baada ya kuondolewa kwenye usemaji wa CCM aliwahi kunukuliwa kwenye mahojiano akisema CCM kumejaa watu wahuni wanaofanya matendo mabaya kama fitina, zengwe na uchawi, dhidi ya watu 'walionyooka' kama yeye na kudai hawezi kupatwa na uchawi hata shetani anamuogopa. Linalongojewa sasa ni kuona mustakabali wake kisiasa baada ya kujiuzulu ubalozi na nafasi nyingine za umma.
0 Comments