Marcelina Mkini mwenyekiti UWT wilaya ya Mufindi
MWENEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, Marcelina Mkini, ametoa wito kwa Watanzania wote, hususan wanawake, kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuendeleza maendeleo ya Taifa.
Akizungumza na Matukio Daima media katika maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania, Mkini alieleza kuwa uhuru ni dhamana kubwa inayopaswa kuheshimiwa kwa vitendo, hasa kwa kushiriki kikamilifu katika kazi za kijamii na maendeleo.
Maadhimisho ya mwaka huu yamekuwa ya kipekee kwa sababu Serikali imeamua kuachana na sherehe za kifahari na badala yake kuelekeza fedha kwenye miradi ya kijamii, ikiwemo afya, elimu, na miundombinu.
Kuwa uamuzi huo, unaoendana na kauli mbiu ya “Uhuru ni kazi,” ni sehemu ya falsafa ya Rais Dkt. Samia ya kuhakikisha kila shilingi inayoelekezwa katika matumizi ya umma inaleta tija kwa wananchi wote.
Mkini alisema Rais Dkt. Samia ameonyesha mfano wa kuigwa kwa kutilia mkazo maendeleo ya watu badala ya matumizi yasiyo ya lazima
"Rais wetu ni muumini mkubwa wa maendeleo hii ndio sababu ameamua kuelekeza fedha zilizotengwa kwa ajili ya sherehe hizi kwenye miradi ya kijamii ambayo italeta matokeo chanya kwa muda mrefu," alisema Mkini.
Aidha, Mkini alisisitiza kuwa Umoja wa Wanawake Tanzania una wajibu wa kuhakikisha unamsemea Rais Samia kwa kazi nzuri anayoifanya.
Hivyo aliwataka wanachama wa UWT kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo kwa vitendo ili kuonesha shukrani kwa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi.
Kuwa katika miaka 63 ya Uhuru, Tanzania imepiga hatua kubwa katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Alisema kuwa mmafanikio haya yanajumuisha uimarishaji wa sekta ya afya, ambapo huduma za msingi zimeboreshwa, sekta ya elimu kwa kuanzisha mpango wa elimu bila malipo, na uboreshaji wa miundombinu kama barabara, reli, na usambazaji wa umeme vijijini.
Rais Dkt. Samia amekuwa chachu ya mafanikio haya kwa kuonesha uongozi wa kipekee unaoendana na mahitaji ya dunia ya sasa.
Kupitia diplomasia ya uchumi, ameimarisha mahusiano ya kimataifa, kuvutia uwekezaji, na kuongeza kasi ya maendeleo ya viwanda.
"Hatuwezi kupuuza kazi nzuri inayofanywa na Rais wetu ni jukumu letu sisi wanawake, kama mhimili wa familia na jamii, kuonyesha mshikamano kwa kufanya kazi kwa bidii," alisisitiza Mkini.
Kwa kuunga mkono falsafa ya Rais Dkt. Samia, Mkini aliwataka wanawake kote nchini kujivunia uhuru kwa vitendo kwa kushiriki katika shughuli za ujasiriamali, kilimo, na sekta nyingine zinazochangia uchumi wa Taifa.
Mkini alisema kuwa kila mwanachama wa UWT ana jukumu la kuwa balozi wa maendeleo kwa vitendo katika maeneo yao.
Katika hitimisho lake, Mkini alisema kuwa miaka 63 ya Uhuru ni fursa ya kuenzi mapambano ya waasisi wa Taifa kwa kuhakikisha tunaendeleza amani, mshikamano, na maendeleo endelevu.
Aliwataka wanachama wa UWT kuungana bega kwa bega na Rais Dkt. Samia katika safari ya kuijenga Tanzania ya kisasa na yenye ustawi.
Kuwa kwa maadhimisho haya ya kihistoria, kila Mtanzania anatakiwa kutambua kuwa uhuru unaenda sambamba na wajibu wa kujituma na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Alisema kuwa kwa kufanya hivyo ni ndio njia bora ya kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake wa busara na wenye maono makubwa kwa mustakabali wa Taifa.








0 Comments