Header Ads Widget

MIAKA 63 YA UHURU: VIJANA TUJENGE TAIFA KWA KAZI NA UZALENDO -TONGA

  


Na Matukio Daima media 

Taifa lipo kwenye maadhimisho ya Miaka 63 ya Uhuru kama ilivyo ada toka Mwaka 1961 nchi ilipopata Uhuru wake hivyo Kila ifikapo Desemba 9, Watanzania husherehekea kumbukumbu ya uhuru wa Taifa lao.

 Mwaka huu, tukiadhimisha miaka 63 tangu uhuru wetu, ni wakati muhimu kwa vijana kutafakari nafasi yao katika maendeleo ya nchi.

 Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Iringa, Agrey Tonga, ametoa wito kwa vijana kujenga Taifa kwa kazi na uzalendo, akisisitiza kuwa uhuru tulionao ni matunda ya juhudi za waasisi wetu, hususan Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na wengineo waliopigania haki ya kujitawala.


Mwenyekiti Tonga ameonesha fahari ya vijana kushuhudia maadhimisho haya, akisisitiza kwamba miaka 63 ya uhuru ni ushuhuda wa kazi nzuri ya viongozi wa awamu zote zilizopita. 

Ametoa mwito wa wazi kwa vijana kuendeleza jitihada hizo kwa kushirikiana na Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan. 


Alisema kuwa, “kazi kwa juhudi na maarifa ni jukumu letu sote vijana katika kuhakikisha tunakuza uchumi wa Taifa na kuimarisha maendeleo ya jamii.”

Serikali ya Awamu ya Sita imeonyesha dhamira ya dhati katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu, huduma za kijamii kama afya, elimu, na maji, pamoja na uwekezaji wa viwanda. 

Tonga amesisitiza kwamba jukumu la vijana ni kuhakikisha miradi hii inalindwa, inahifadhiwa, na kutumika kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.

 “Serikali inatekeleza miradi mingi ya maendeleo, jukumu letu vijana ni kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi hiyo na kuhakikisha inaleta tija kwa wananchi,” aliongeza.


Kwa mfano, miradi kama Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), na madaraja makubwa kama lile la Tanzanite, ni fursa kwa vijana kushiriki moja kwa moja kama wafanyakazi, wasimamizi, na walinzi wa rasilimali za Taifa. 

Tonga alihimiza vijana kutumia miradi hii kama jukwaa la kujifunza, kubuni teknolojia mpya, na kujenga ustawi wa kiuchumi.

Alisema kuwa Tanzania ni nchi inayojivunia amani na mshikamano wake tangu uhuru.

Hivyo  Tonga alieleza kuwa moja ya mafanikio makubwa ya miaka 63 ya uhuru ni utulivu wa kisiasa na kijamii ambao umekuwa nguzo ya maendeleo yetu. Amehimiza vijana kuhakikisha wanadumisha hali hiyo kwa nguvu zote.

 “Hakuna maendeleo bila amani,” alisema, akiongeza kwamba vijana wana jukumu la kuhakikisha wanajiepusha na vitendo vyote vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi.

 Tonga alisema kuwa  vijana wanapaswa kuwa daraja la mshikamano na upatanisho.

 “Kama taifa, hatuwezi kuendelea bila mshikamano. Vijana ndio nguvu kazi ya Taifa; ni lazima tuoneshe mfano wa uzalendo kwa kuepuka chuki na migawanyiko,” alisema.

Tonga aliwahimiza vijana kushiriki katika shughuli za ujasiriamali, ambazo zina mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa mtu binafsi na wa Taifa kwa ujumla.

 Alisisitiza kuwa serikali imeweka mazingira rafiki kwa vijana kuanzisha na kuendesha biashara ndogo na za kati kupitia mifuko ya uwezeshaji kama Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.

Hata hivyo alibainisha kuwa kwa kujihusisha na ujasiriamali, vijana wataweza kujiajiri, kukuza pato la Taifa, na kupunguza utegemezi.

Aliwataka vijana kutumia ubunifu wao kubuni suluhisho za changamoto zinazolikabili Taifa, hususan katika sekta za kilimo, teknolojia, na huduma za kijamii.

 Alisema kuwa ujasiriamali wa vijana ni kichocheo cha maendeleo ya uchumi jumuishi, na ni lazima vijana wawe tayari kuchangamkia fursa zilizopo kwa bidii na maarifa.

Mwenyekiti huyo  aliwataka vijana kuimarisha mshikamano miongoni mwao kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kijamii na kijamii katika kuleta maendeleo.

 Pia alisositiza  umuhimu wa vijana kujiunga na vikundi vya kijamii, vyama vya ushirika, na asasi za kiraia kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na maarifa.


“Umoja ni nguvu. Vijana tukishirikiana kwa pamoja, tunaweza kufanikisha mambo makubwa. tusikubali kugawanywa kwa misingi ya vyama, dini, au ukabila. 

Kuwa Tanzania ni yetu sote, na kila mmoja anapaswa kuchangia maendeleo yake,” alisema.

Hata hivyo Tonga aliwakumbusha vijana kwamba uzalendo ni moyo wa kujituma kwa ajili ya nchi bila kujali changamoto zinazokabiliwa. 

Kuwa uzalendo wa kweli hujidhihirisha katika maadili mema, heshima kwa sheria, na kujituma kwa ajili ya ustawi wa jamii.

 “Tusisahau kuwa miaka 63 ya uhuru wetu ni matokeo ya uzalendo wa waasisi wetu. Hili ni somo kwetu kwamba hakuna maendeleo bila kujituma na kuwa na maadili thabiti,” alisema.


Alisema  vijana wote nchini kutumia maadhimisho haya kama fursa ya kujitathmini, kujifunza, na kuahidi kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya kuijenga Tanzania mpya yenye uchumi imara na jamii yenye mshikamano.

Maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa Tanzania ni wakati wa kukumbuka historia yetu, kusherehekea mafanikio, na kupanga hatua za mbele. 

Vijana, wakiwa ndiyo nguzo kuu ya maendeleo ya Taifa, wanapaswa kuchukua nafasi yao kwa uzito katika kujenga uchumi, kulinda amani, na kudumisha mshikamano. 

Kwa kufanya kazi kwa bidii na kwa uzalendo, vijana wa Tanzania watahakikisha kwamba uhuru tulioupata unazidi kuwa na maana kwa vizazi vijavyo.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI