Na Thobias Mwanakatwe,DODOMA
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Ashatu Kijaji,amewataka wataalamu katika wizara hiyo kushirikiana katika kuwahudumia wafugaji na wavuvi ambao ndio wazalishaji wakuu wa uchumi katika sekta hiyo.
Alisema hayo jana wakati wa hafla ya makabidhiano ya nyaraka za ofisi baina yake na mtangulizi wake, Abdallah Uledi iliyofanyika makao makuu ya wizara hiyo, mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.
“Kaka yangu Ulega amefanya kazi kubwa ya kuipaisha wizara hii na mimi nitaendelea kujifunza kutoka kwako ili niweze kukimbia na kasi ambayo mheshimiwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassa anaitaka kwani sekta ya mifugo na uvuvi ina mchango mkubwa zaidi kwenye pato la taifa," alisema.
Dk. Kijaji ameongeza kuwa dhamira yake ni kuona sekta za Mifugo na Uvuvi zinakuwa miongoni mwa sekta muhimu katika ustawi wa uchumi wa Wananchi na taifa kwa ujumla.
Naye aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambaye kwa sasa ni Waziri wa Ujenzi,Abdallah Ulega, alisema kwa kipindi cha miaka saba ndani ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wataalamu wamefanikiwa kuiweka Wizara hiyo kwenye twasira ya kitaifa kupitia miradi mikubwa iliyozinduliwa na Rais Dkt Samia.
"Mhe Waziri kitu ambacho ninajivunia katika miaka saba kwenye wizara hii ni utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko na ule wa ugawaji wa Vizimba na Boti kwa wavuvi hapa nchini kwa sababu ni miradi ambayo imekwenda kugusa wananchi moja kwa moja," alisema.
Ulega aliwataka wataalamu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kumpa ushirikiano Dk. Kijaji ili aweze kuisaidia wizara kufanikisha usimamiaji wa miradi ili kuleta tija kwa Wananchi.
Awali akizungumza kwenye makabidhiano hayo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe alisema Wizara itaendeleza maono ya Mhe Ulega katika kutekeleza majukumu ya wizara katika kukuza ustawi wa sekta za mifugo na uvuvi huku akimshukuru Waziri huyo kwa uongozi wake.
0 Comments