Header Ads Widget

DC ITUNDA MGENI RASMI BONANZA LA MWAKA MPYA, MULUGO AMWAGA ZAWADI.

Na Moses Ng'wat, Mkwajuni.

MASHABIKI wa michezo Wilayani Songwe wanatarajia kuukaribisha mwaka mpya wa 2025 kwa  burudani ya kipekee kupitia bonanza kubwa.

Bonanza hilo litahusisha mchezo wa soka kati ya mashabiki wa vilabu viwili vikubwa hapa nchini vya Yanga na Simba limeandaliwa na Mbunge wa jimbo la Songwe, Philipo Mulugo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mbunge Mulugo ambaye ndiye mratibu wa bonanza hilo, litafanyika Januari Mosi 2025 katika viwanja vya Mkwajuni Centre kuanzia majira ya saa tisa alasiri.

Kwa mujibu wa Mulugo,  mechi hiyo itakuwa na zawadi nono kwa washindi, ambapo mshindi wa kwanza ataondoka na Shilingi 400,000, huku mshindi wa pili akipata Shilingi 200,000.

Mbali na zawadi hizo, kutakuwa na tuzo maalum kwa wachezaji bora katika vipengele vya mfungaji bora, kipa bora, mchezaji bora mwenye nidhamu, na burudani nyinginezo.

Mbunge Mulugo amesema tayari timu zote mbili  zimeanza mazoezi, zikiwa zimepewa mipira mipya kama sehemu ya maandalizi.

Aidha, Mbunge Mulugo ameweka wazi kuwa gharama nyinginezo muhimu za mchezo tayari zimelipwa kupitia chama cha soka cha Wilaya ya Songwe (SODIFA, huku akitoa wito kwa timu shiriki kujisimamia kwenye jezi za mchezo huo.

Bonanza hilo linatarajiwa  kupambwa na burudani kutoka kwa wasanii wa ndani ya Wilaya ya Songwe, ambapo wapenzi wa michezo na burudani watapata nafasi ya kufurahia siku ya kipekee.

Mgeni rasmi wa tukio hilo anatarajiwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Solomon Itunda ambaye pia atatoa hotuba ya kufungua rasmi mwaka mpya wa 2025.

Mulugo amewataka wanamichezo wote, hasa mashabiki wa Simba na Yanga, kujitokeza kwa wingi kushangilia na kuonyesha mshikamano wa kweli.

 “Hii ni nafasi yetu kama wanaSongwe kuonyesha mshikamano kupitia michezo".





 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI