Na Matukio Daima media
MWENYEKITI wa Chama Cha mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa Daud Yassin amesema kuwa Matokeo ya Uchaguzi wa serikali za mitaa na ushindi uliopatikana ni kazi nzuri ya wana CCM wote .
Alisema ushirikiano mkubwa uliooneshwa na Wana CCM wakati wa Kampeni na Uchaguzi ndio umekiwezesha Chama hicho kuibuka na ushindi .
Kwani alisema katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji, na Vitongoji wa mwaka 2024 ushindi wa CCM mkoani Iringa ni ushindi wa kihistoria unaoashiria mshikamano, maandalizi bora, na utekelezaji thabiti wa Ilani ya CCM.
Yassin amesema kuwa ushindi huu si wa wana CCM wa mkoa wa Iringa pekee, bali ni wa familia nzima ya chama kote nchini.
Kuwa Kazi kubwa sasa ni kuhakikisha viongozi waliochaguliwa wanatekeleza kwa ufanisi ilani ya CCM kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Ikumbukwe kuwa mkoa wa Iringa una jumla ya vijiji 360, mitaa 222, na vitongoji 1,840.
Katika uchaguzi wa mwaka huu, vyama vya upinzani vilijitokeza kuwania vijiji 104, mitaa 50, na vitongoji 333 pekee.
Hata hivyo, matokeo ya mwisho yalionesha nguvu ya CCM katika kusimamia maandalizi ya uchaguzi.
CCM ilifanikiwa kushinda vijiji vyote 360, mitaa yote 222, na vitongoji 1,839. Kitongoji kimoja tu ndicho kilipotezwa kwa wapinzani, hali inayoifanya CCM kufanikisha ushindi wa asilimia 99.99.
"Ushindi huu mkubwa ni kiashiria wazi cha imani ya wananchi kwa chama ni matokeo ya juhudi za pamoja za viongozi, wanachama, na mashabiki wa CCM katika kuhakikisha kuwa chama kinapata ushindi wa kishindo"
Yassin alibainisha kuwa ushindi huu umetokana na maandalizi makini yaliyofanywa na chama.
"CCM ilihakikisha kuwa inasimamia kikamilifu utekelezaji wa Ilani yake, jambo lililojenga imani miongoni mwa wananchi"
Pia Miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu imekuwa daraja la kuimarisha mahusiano kati ya chama na wananchi wa Iringa.
Aidha, maandalizi ya uchaguzi yalijumuisha usimamizi wa karibu wa shughuli za chama, kuimarisha uhamasishaji wa wanachama, na kuhakikisha kuwa wagombea walioteuliwa walikuwa wenye uwezo wa kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na bidii.
Mbali na hayo, CCM ilijipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa inashirikiana na jamii kwa karibu ili kuelewa changamoto zao na kutafuta njia bora za kuzitatua.
Yassin alisema mbali ya kuwashukuru Wana CCM wote kwa kukipigania Chama kupata ushindi pia anawapongeza viongozi wote akiwemo MNEC Salim Abri Asas,wabunge wote ,madiwani na viongozi wote wa mkoa wa Iringa kwa Kila mmoja kuwajibika kuona Chama kinashinda.
Alisema baada ya ushindi huu, CCM mkoani Iringa inalenga kuhakikisha kuwa viongozi waliochaguliwa wanatekeleza ahadi walizotoa wakati wa kampeni.
Mwenyekiti Yassin alisema kuwa kazi ya viongozi sasa ni kutekeleza Ilani ya CCM kwa vitendo na kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi katika kila kona ya mkoa.
"Ushindi huu pia umeweka msingi mzuri wa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, ambapo CCM inalenga kuendelea kuongoza kwa kutegemea imani ya wananchi na rekodi ya utekelezaji bora wa miradi ya maendeleo"
Kuwa ushindi wa CCM katika mkoa wa Iringa si tu ushindi wa idadi bali pia ni ushindi wa imani na matumaini ya wananchi.
"Ni ushindi unaothibitisha kuwa CCM imejipanga vyema kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuhakikisha maendeleo ya kweli yanawafikia wananchi"
Kuwa ushindi huu wa asilimia 99.99 unatoa hamasa kwa chama kote nchini kuendelea kujipanga na kuhakikisha mafanikio haya yanadumu hadi uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na zaidi.
Hivyo wananchi wa Iringa wameonesha kuwa wana imani na CCM, na sasa ni jukumu la viongozi walioteuliwa kuthibitisha kuwa imani hiyo haikuwa ya bure.
0 Comments