Header Ads Widget

BIBI WA MIAKA 70 AJERUHIWA KWA KUKATWA MAPANGA NA MWANAYE

 


BIBI mmoja Unni Martin (70,) mkazi wa Kitongoji cha Gudugudu kata ya Mlali wilayani Mvomero Mkoani Morogoro amejeruhiwa kwa kukatwa katwa na panga na Mwanaye wa kiume, Elias Paulo (38) anayedaiwa kusumbuliwa na changamoto ya ugonjwa wa akili.

Majeruhi huyo aliyejeruhiwa maeneo ya mkono, kichwani na mguuni na amelazwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu.

Muuguzi wa zamu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro Bw Frank Kalinga alisema majeruhi huyo amefikishwa hospitalini hapo akitokea kituo cha afya cha Mlali na kwamba baadhi ya majeraha yake yalikuwa bado yanavuja Damu.

"Hata hivyo kwa sasa majeruhi huyu anaendelea vizuri na matibabu"Alisema Kalinga.

Mapema mke wa mtuhumiwa huyo Bi Evarista Matei alisema mume wake alikuwa akisumbuliwa na changamoto ya ugonjwa wa akili kwa muda mrefu lakini hapa katikati baada ya matibabu tatizo hilo lilikuwa limetulia.

"Usiku wa kuamkia Desemba 06 alikuwa akiongea mambo ya ajabu ajabu hata siyaelewi, kulipokucha nikamsihi twende hospitali akakubali, lakini huko alikataa kuchomwa sindano na akaondoka kuja kumshambulia mama yake kwa Panga"Alisema mwanamke huyo.

 Alisema baada ya tukio hilo, mama wa mumewe alipoteza fahamu na Mume wake aliondoka na yeye kupiga kelele kuomba msaada wa majirani waliofika na kumkimbiza majeruhi kituo cha afya cha Mlali kwa matibabu, kabla ya kumhamishia hospitali ya Rufaa ya mkoa.

Kaka wa mtuhumiwa Paulo Paulo akizungumzia tukio hilo  linalodaiwa kutokea Desemba 06 mwaka huu, majira ya saa nne asubuhi, alikiri  ndugu yake kwa kipindi cha nyuma alishawahi kukabiliwa na changamoto ya ugonjwa wa akili kulikochangiwa na matumizi ya madawa ya kulevya .

Akadai tatizo hilo lilichangiwa na  uvutaji wa bangi lakini alipewa matibabu kwa karibu miaka  saba iliyopita na kuacha kabisa uvutaji ingawa tukio la kumshambulia Mzazi wake linaonesha huenda bado alikuwa akivuta na hajaacha.

 Akasema ingawa mwenyewe mtuhumiwa alikuwa akikana kuendelea kuvuta lakini majirani walisema alikuwa anaendelea kuvuta madawa hayo na baada ya kumshambulia mama yao alikimbia na baadae kurudi tena nyumbani na kuanza kufukia damu za majeruhi..

Mwenyekiti wa kitongoji cha Gudugudu kata ya Mlali Bw Iddi Hassan alisema baada ya kupata taarifa za tukio hilo majira ya saa nne asubuhi aikwenda eneo la tukio na kumkuta mama huyo akiwa amefichwa nyuma ya nyumba ili asiendelee kudhuriwa zaidi huku damu zikiwa zinamwagika kutoka kwenye majeraha yake.

Akasrma Miaka ya nyuma kijana huyo mtuhumiwa naye aliwahi kushambuliwa kwa mapanga na wananchi akiwa kwenye kijiji cha jirani baada ya kurukwa na akili na kufanya matendo yaliyozua sintofahamu na kuonekana huenda alikuwa mwizi.

Mwenyekiti huyo akasema licha ya mtuhumiwa kukimbia baada ya tukio,vijana  kijijini hapo walimtafuta na kumkamata na kumpeleka Polisi kwa hatua zaidi.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI