Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WATOTO 100,000 waliokosa elimu au kukatisha masomo wanatarajia kurudishwa shuleni wakinufaika na mpango unaosimamiwa na SHIRIKA la Umoja wa mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) na serikali ya Tanzania.
Afisa elimu wa Shirika la UNICEF mkoa Kigoma, Farida Sebarua akizungumza katika uzinduzi wa mpango huo mkoani Kigoma alisema kuwa mpango huo unaojulikana kama Elimisha Mtoto unatekelezwa katika mikoa ya Tabora,Songwe na Kigoma kwa miaka mitano kuanzia 2022 hadi 2027.
Sebarua alisema kuwa sababu kubwa ya kutekelezwa kwa mpango huo katika mikoa hiyo mitatu inatokana na utafiti uliofanywa mwaka 2021 unaoonyesha kwamba mikoa hiyo mitatu ina changamoto kubwa ya wanafunzi kutomaliza elimu yao ya Msingi (utoro sugu) na wengine kutoanza masomo kabisa.
Mpango huo unatelelekezwa kupitia Mpango maalum wa ufadhili wa serikali ya Qatar unaofahamika kwa jina la Educat Above All unaojikita kuhakikisha wanafunzi wote walio na umri wa miaka saba hadi 15 wanaanza masomo hivyo ambayo hawajaanza masomo watatafutwa, kuandikishwa na kuanza masomo ikiwemo pia walioanza masomo na kukatisha masomo yao.
Akizundua mpango huo kwa mkoa Kigoma Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye alisema kuwa mkoa Kigoma unakabiliwa na changamoto kubwa ya wanafunzi kutoanza masomo lakini pia kuwepo na wanafunzi wanaokatisha masomo.
Takwimu za mwaka 2023/2024 zinabainisha kuwa Watoto 12,517 waliandikishwa kuanza masomo katika mfumo usio rasmi kutokana na kutoanza masomo kabisa huku mwaka huu takwimu zikionyesha kukiwa na Watoto 7475 ambao hawapo katika mfumo wa elimu wakati walipaswa kuwa shuleni wakati huu.
Andengenye alisema kuwa kutokana na hilo serikali ya mkoa kupitia kwenye halmashauri za mkoa huo kwa mwaka 2025 imedhamiria kuandikisha Watoto 5632 ili kuwarejesha katika mfumo usio rasmi waweze wapate elimu sambamba na kuwarudisha shuleni Watoto 2001 ambao wamekatisha masomo (utoro sugu).
Changamoto hiyo inaelezwa kuchangiwa na mambo mbalimbali ikiwemo Umasikini wa wazazi, mwamko mdogo wa jamii kuhusu umuhimu wa elimu na hivyo kuwatumia Watoto kwenye kazi za vibarua badala ya kuwapeleka shule,mila potofu na hofu ya adhabu za viboko.
0 Comments