Header Ads Widget

FADHIL NGAJILO AJITOLEA KUJENGA DARAJA LA KINEGAMGOSI KATA YA RUAHA,WANANCHI WAMPONGEZA



Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi wa Chama Cha mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa Fadhil Ngajilo (wa pili kulia)na mjumbe wa kamati ya utekelezaji Jumuiya hiyo mkoa Hosea Kabelege kushoto walishiriki ujenzi wa Daraja la Kinegamgosi kata ya Ruaha Leo na wananchi wa kata hiyo 
Na Matukio Daima media 

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Fadhili Ngajilo amejitolea kuwajengea daraja la kinegamgosi wakazi wa kata ya Ruaha Manispaa ya Iringa ambao walikuwa wakisumbuka kutokana na daraja Hilo kusombwa na mvua mwaka Jana .

Mwenyekiti huyu amewaunga mkono wananchi hao kwa Kwa kutoa  msaada wa saruji, mawe, na fedha kwa ajili ya kulipa mafundi wanaoshiriki katika ujenzi huo.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya kushirikishwa na Diwani wa Kata ya Ruaha, Tandes Sanga, pamoja na kujionea juhudi za wananchi katika kutekeleza mradi huo muhimu. 


Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Ngajilo alisema kukamilika kwa daraja hilo kutasaidia kupunguza changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi wa eneo hilo, hasa katika usafiri na usalama.

Ngajilo pia aliwataka wananchi kuacha tabia ya kusubiria serikali pekee katika miradi ya maendeleo, akisisitiza kwamba wao pia ni sehemu muhimu ya serikali na wanapaswa kuchangia kwa namna mbalimbali katika miradi ya kijamii.

Aidha, Mwenyekiti huyo aliwakumbusha wazazi kuwa makini na matumizi ya daraja hilo kwa watoto ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika, hasa wakati wa mvua na maji mengi.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ruaha, Tandes Sanga, alieleza kuwa daraja hilo limekuwa ni kero ya muda mrefu kwa wananchi, likikwamisha shughuli za maendeleo na kijamii. 

Sanga alimshukuru Fadhili Ngajilo kwa msaada wake na wananchi wa Kata ya Ruaha kwa jitihada zao. Aliongeza kuwa kutokana na juhudi hizo, ujenzi wa daraja hilo unatarajiwa kukamilika ndani ya wiki mbili zijazo.


Wananchi wa Kata ya Ruaha walimpongeza Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM, Fadhili Ngajilo, kwa kujitoa na kuona umuhimu wa kuwaunga mkono katika mradi huo. 

Walisema kukamilika kwa daraja hilo kutaboresha maisha yao, hasa kwa watoto ambao wamekuwa wakipata changamoto kubwa kuvuka eneo hilo.

Ujenzi wa daraja hilo unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa kwa wananchi, ikiwemo kuboresha usalama na kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii katika Kata ya Ruaha.






Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI