Na Matukio Daima App.
Wakulima wa zao la Pamba katika Kijiji cha Mandang'ombe wilayani Maswa Mkoani Simiyu wamepata mafunzo ya Uandaaji wa Mbolea Ukaa ili waweze kuitumia katika kuongeza tija ya uzalishaji wa zao la Pamba.
Akizungumza wakati wa Mafunzo hayo, Mwezeshaji wa Kampuni ya Alliance Ginnery, Martin Simasiku kutoka nchini Zambia amesema Mafunzo hayo yanatolewa kwa wakulima ikiwa ni Mwendelezo wa Mkakati wa Bodi ya Pamba kuongeza rutuba ili kupata tija ya Pamba.
"Tunatoa Mafunzo haya kwa wakulima ili kutekeleza Mkakati wa Bodi ya Pamba wenye lengo la kuongeza rutuba kwenye udongo ili kupata tija ya zao la pamba" amesema Martin.
Kwa mujibu wa Bodi ya Pamba nchini (TCB), wameeleza kuwa Wakulima wa wilaya nane za kimkakati ambazo ni Bariadi, Busega, Itilima, Meatu, Maswa, Bunda, Igunga na Kishapu wanatarajia kunufaika na Mafunzo hayo.
Imeelezwa kuwa Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Biashara (ITC) kupitia Mradi wa uongezaji Tija na Thamani ya zao la Pamba.
Mbolea ya Ukaa *(Bio-Char)* hutengenezwa kwa kutumia masalia ya mazao mbalimbali kama vile Pamba, Alizeti, Mahindi na kwamba imebainika kuwa na manufaa katika kuzuia upotevu wa virutubisho vya udongo na kutunza unyevu.
0 Comments